GERALD Mdamu, mshambuliaji wa Mwadui FC yupo mbioni kujiunga na Polisi Tanzania ili kuziba nafasi ya Ditram Nchimbi aliyesajiliwa na Yanga kwa kandarasi ya miaka miwili.
Mdamu alipata umaarufu baada ya kuifunga Simba kwenye mchezo wa saba uliochezwa uwanja wa Kambarage ikiwa ni mechi ya kwanza kupoteza kwa mnyama ambaye alicheza mechi sita za ligi nyuma bila kufungwa.
Habari zinaeleza kuwa Mdamu mwenye mabao manne alikuwa anawindwa na Yanga ambao walikuwa kwenye mazunguzo naye ya mwisho waliachana naye baada ya kumpata Nchimbi ambaye wameshamalizana naye jambo lililowapa nafasi Polisi Tanzania kulipa kisasi kwa kuinyaka saini yake.
"Kwa sasa Polisi Tanzania inafanya mchakato wa kumpata mbadala wa Nchimbi mwenye mabao manne, Mdamu amewekwa kwenye hesabu na muda wowote wakimalizana atatangazwa ndani ya Polisi Tanzania kuwa mshambuliaji wao mpya," kilieleza chanzo hicho.
Frank Lukwaro, Ofisa Habari wa Polisi Tanzania amesema kuwa wapo kwenye mwendelezo wa kusuka kikosi hicho kwa sasa kwa kuwatafuta wachezaji wenye uzoefu.
"Tunahitaji wachezaji makini na bado usajili unaaendelea aliyetufungulia milango ni Pius Buswita wengine wanakuja, mashabiki wasiwe na mashaka, suala la Mdamu lipo mezani linafanyiwa kazi" amesema.
0 COMMENTS:
Post a Comment