MZUNGUKO wa kwanza bado unaendelea kwenye Ligi Kuu Bara ambayo kwa sasa imezidi kuwa na ushindani kutokana na kila timu kusaka ushindi ndani ya uwanja.
Kuna mengi
ambayo yanatokea ndani ya uwanja na nje ya uwanja ni muhimu kujifunza na
kuongeza ubora zaidi kwa yale ambayo yamepita na yale ambayo yanaendelea kwenye
soka letu la Bongo.
Pongezi kwa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuweza kuweka usawa kidogo katika ratiba
msimu huu kwa kuwa hakujawa na viporo vingi labda ni kwa sababu msimu huu timu
zetu zimeishia hatua ya awali kwenye Ligi ya Mabingwa hii ni mbaya kwetu kwa
msimu huu kwa kushindwa kupenya kimataifa.
Kwa mapenzi
ya Mungu tumeweza kuonana tena ndani ya mwaka mpya 2020 ni jambo la kushukuru kwa kweli kwani yeye ndiye anayetulinda na kutupigania hivyo tunapaswa tushukuru
kwa yote ambayo yametokea kwa mwaka uliopita.
Maumivu
makubwa ambayo tuliyapata mwaka jana 2019 hasa kwa upande wa kimataifa kwa kuwa
hakuna timu iliyofanya vema zote ziliboronga jambo ambalo limetufanya tuwe na usimanzi mwaka huu mambo yawe mengine kabisa ya kutafuta mafanikio.
Timu yetu
ya Taifa chini ya miaka 17, Serengeti Boys iliboronga kwenye michuano ya Cecafa
iliyoandaliwa na TFF ni jambo baya kwetu kulirudia tena ama kulisahau bila
kulifanyia kazi kwa kutafuta majibu yake mwaka huu mpya.
Yale makosa
ambayo yalitukosesha furaha mwaka uliopita tuachane nayo tutafute majibu sahihi
ambayo yatatufanya tuwe imara muda wote kwenye michuano ambayo tunaandaa ama
kualikwa na kufanya kweli ndani ya mwaka 2020.
Hakuna
kukumbuka mafanikio kisha ukadhani utafanikiwa muda wote ndani ya mwaka 2020
bila kutafuta majibu kwa yale uliyofeli itakuwa ni uongo wa karne hivyo kwenye
soka haupaswi kupewa kipaumbele.
Tusisahau
kwamba hata timu ya Taifa ya Wanawake, Kilimanjaro Queens nayo pia iliboronga
ikiwa nyumbani kwa kushindwa kuifunga Kenya kwenye mchezo wa fainali wa Cecafa
iliyofanyika hapahapa Bongo tena uwanja wa Chamazi na lundo la mashabiki.
Katika yale
makombe ambayo tulikuwa wenyeji msimu uliopita tuliboronga na kuweka rekodi
mbovu ambayo inapaswa sasa itafutiwe majibu ndani ya mwaka 2020 ambao tumeanza
ukurasa mpya.
Michezo
mingine ambayo imekuwa ikitubeba imekuwa haipewi kipaumbele kikubwa licha ya
watanzania kupambana kufanya vizuri ni wakati wa kutazama nini tutafanikiwa
kuinua zaidi ya pale tulipokuwa.
Hapo kuna
mchezo wa ngumi ambao umeanza kurejea kwenye ubora wake ni muda wa kutazama
namna gani tunaweza kufikia malengo ya kuwa juu kuliko hapa tulipo.
Yale mazuri
ya TFF yanapaswa yaongezwe zaidi kwenye utendaji na kufanya utekelezaji ule
unaoonekana kwani stori kwenye soka huwa hazijengi vitendo ndio kitu cha msingi
katika hili.
Taifa
linahitaji kuona kwamba hakuna mambo ya kuchanganya siasa na mpira kwa zama
hizi zaidi ya kuangalia namna gani tunajipanga kuleta ushindani katika kile
ambacho tunakifanya.
Wachezaji
wana jukumu la kufanya tathimini ya kile ambacho walikifanya ndani ya uwanja
kwa mwaka uliopita kama kinaendana na uwezo wao pamoja na timu ambayo
wanaitumikia.
Mashabiki
nao mwaka huu wanatakiwa wabadili mfumo wa ushabiki sio wanajitokeza uwanjani
kuzomea pale wapinzani wao wanaposhindwa kufanya vizuri na kuishia kushangilia
chenga na mabao kisha muda mwingine wanakaa kimyaa hii ni mbaya.
Kila mmoja
afanye kazi kwa umakini na kwa wajibu kwa mwaka huu nina amini ndugu msomaji itakuwa
rahisi kuyafikia malengo ambayo tumejiwekea kiujumla kwenye uwanja wa soka
letu.
Sasa ngoja
twende kule ambako nilikuwa nimelenga leo kuzungumzia kwa upana ni kuhusu
ushindani uliopo kwenye Ligi Kuu Bara ambayo inaendelea kwa sasa.
Hali halisi
tunaiona kwa sasa jambo ambalo limepamba moto ni mchezo wa watani wa jadi ambao
ni Simba na Yanga utakaochezwa uwanja wa
Taifa.
Tayari
vuguvugu limesambaa na kila kona ni wimbo mmoja tu mechi ya Simba na Yanga
ambazo zitapambana ndani ya uwanja hivi karibuni na kuendeleza mchezo wa ligi.
Kila timu
inapambana kwa namna inavyoweza kuweza kujiweka rekodi yake ndani ya mwaka mpya
wa 2020 kwenye mechi zao za mwanzo jambo jema kusaka ushindi wa halali na sio
ujanjaujanja.
Hakuna
mwalimu duniani ambaye anaingia Uwanjani akiwa anafikiria kufungwa, sasa kama
ipo hivyo basi hata mbinu za kutafuta ushindi zinapaswa zibadilike.
Tunahitaji
kuona soka safi na kila mchezaji ndani ya uwanja aonyeshe sababu ya kuwa ndani
ya Yanga ama Simba na sio kumtegemea mchezaji fulani ndiye ataokoa jahazi
hakuna kitu hicho kwa sasa.
Sasa ni
wakati mwingine wa kukaza buti na kutumia akili na nguvu kutafuta matokeo
chanya kwenye michezo yote ya ligi ikiwa ni pamoja na huu utakaochezwa Jumamosi
ambao utavuta hisia za wengi zaidi.
Uzuri ni
kwamba mshindi wa mechi hii hatabiriki haijalishi nani yupo vizuri kifedha ama
kitimu hakuna kinachomata katika mechi hii zaidi ya kuangalia maandalizi halisi
ya wachezaji.
Ushindani
ukiwa mzuri ni nafasi yetu hasa kutengeneza timu bora ya Taifa hasa na
kufanikiwa kuibua vipaji ambavyo ni kwa manufaa yetu wenyewe.
Tuna
wachezaji wa kigeni ambao wanafanya vizuri hao wawe ni chachu kwetu kuongeza
juhudi na kuonyesha uwezo ambao tunao na sio kukimbilia kubeza uwezo wao.
Mwalimu
anapenda kumtumia mchezaji mwenye kubadilisha matokeo muda ambao hakuna shabiki
anayeamini kwamba kuna jambo litatokea.
Hicho
ndicho ambacho mchezaji anapaswa afanye hasa akiwa uwanjani, juhudi zake na
kujituma ni faida kwa timu nzima na sio yeye peke yake.
Muda
mwingine timu inapata matokeo mabovu kutokana na kuamini uwepo wa mchezaji
fulani ndani ya kikosi utatusaidia hali inayoleta shida wakati akiwa hayupo.
Wengi bado
hawajajua maisha ambayo tunaishi tunayabeba kwa asilimia kubwa kwenye
saikolojia na maisha yetu hivyo mfumo wetu unavyofikiria kuna jambo fulani
litatokea ndivyo inavyokuwa.
Wachezaji
wote ni muhimu hakuna ambaye ni bora kuliko mwingine zaidi kinachotofautisha ni
nafasi na ule uwezo binafsi wa kulazimisha mambo yatokee Uwanjani.
Basi kama
yote yanawezekana kuna haja ya kufanya mabadiliko makubwa ndani ya uwanja na
nje ya Uwanja kwa kuamini kwamba kila mchezaji ana nafasi ya kubadilisha
matokeo akiwa ndani ya uwanja.
Mashabiki
watakaojitokeza wasiwe na matokeo mikononi mwao hilo litawatesa na kuwaumiza
baadaye ndani ya dakika tisini ndipo ninaamini mshindi atapatikana ama kama
itakuwa ngoma sare hapo ndipo tutapata ukweli wa mambo.
0 COMMENTS:
Post a Comment