January 2, 2020








Na Saleh Ally
WAKATI Ligi Kuu England msimu wa 2019/20 ikiwa ndio mbichi kabisa, Teemu Pukki wa Norwich alionekana ameibuka na mapinduzi mapya.


Alikuwa akifunga mfululizo na kuwafanya wengi kuamini angeshika nafasi hiyo ya waliofunga mabao mengi kwa muda mrefu. Lakini sasa yuko katika nafasi ya 10 akiwa na mabao tisa.


Ilionekana kama Sergio Aguero na mwenzake Harry Kane ambao hushindana mara nyingi wangeibuka na kumkamata Pukki na ikiwezekana kuongoza, sasa wako katika nafasi ya sita kwa Kane mwenye mabao 11 na nane kwa Aguero akiwa na mabao 10.

Ligi bado inaendelea na kuna uwezekano mambo yakabadilika na ambaye bado yuko chini akaibuka na kufunga mabao mengi na kushika nafasi ya juu kabisa.
Hata hivyo, katika Premier League, hakuna zawadi ya mabao, badala yake mshambuliaji analazimika kufanya kazi hasa ili kupata bao moja au mawili.


Kinachoonekana ni kitu tofauti sana na kilichokuwa kikitokea katika EPL misimu mingine. Kwa wanaoongoza msimu wote walio katika tatu bora, mabao yao mengi wamefunga zaidi ugenini.


Yaani washambuliaji hao, wamekuwa bora zaidi na timu zao wanapokuwa na timu za ugenini, jambo ambalo ni tofauti kidogo kwa Pukki, Aguerro na Kane ambao wamekuwa bora zaidi wanapokuwa katika viwanja vyao vya nyumbani.
Katika mabao yake 11, Kane amefunga sita akiwa nyumbani na matano ugenini. Aguero kafunga 10, kati ya hayo sita nyumbani na manne ugenini na Pukki ana tisa, sita akiwa amefunga nyumbani na matatu ugenini.
Hapa unawaona wale walio juu, Jamie Vardy wa Leicester City ambaye aliibuka baadaye kama kimondo ana mabao 17 kileleni mwa wafungaji wanaochuana vikali na kati ya hayo, nane amefunga kwenye Uwanja wa nyumbani wa Kings Power na tisa amefunga akiwa ugenini.


Nafasi ya pili hadi sasa inashikiliwa na Pierre-Emerick Aubameyang ambaye amefunga mabao 13, kati ya hayo matano ndio yamepatikana nyumbani Emirates na nane amefunga katika mechi za ugenini kama ilivyo kwa Tammy Abraham wa Chelsea ambaye amefunga mabao manne tu pale Stamford Bridge na nane akiwa ugenini, kama unakumbuka bao la nane amelifunga akiwa Emirates, Chelsea ikiizamisha Arsenal na kumfanya afikishe mabao 12.
Mabao ni mabao tu, yanahesabika katika idadi ya wafungaji. Lakini inajulikana namna kunavyokuwa na ugumu wa kufunga ugenini.


Timu nyingi zinapokuwa katika viwanja vya nyumbani zinakuwa ngumu sana. Zinapambana kuhakikisha zinashinda na hata aina ya uchezaji inakuwa tofauti kidogo, wenyeji ndio wanakuwa wanasukuma mashambulizi mengi zaidi hivyo kuwafanya wageni wajilinde au kuwa na mashambulizi machache.



Mwendo wa kuonekana wanaoongoza wamefunga ugenini zaidi maana yake, wafungaji wametoa adhabu wakiwa katika viwanja mbali na nyumbani kwao. Hii maana yake kuna kitu kinabadilika katika soka la England na ikiwezekana mifumo.


Kwamba timu zinapokwenda viwanja vya ugenini, zina nafasi ya kupata mabao zaidi kupitia mfumo wa kufunga wa timu nyingi zinapokuwa katika viwanja vya nyumbani kwa kuwa zaidi zinalazimika kutaka kuwafurahisha mashabiki wao lakini hii inakuwa ni hatari zaidi kwao.


Vardy anaonekana pia ni hatari zaidi kuanzia dakika ya 61 hadi 75 kwa kuwa katika muda huo amefunga mabao matano. Hali kadhalika Aubameyang amefunga mabao manne katika muda huo kati ya 13 aliyofunga.


Upande wa Abraham, anaonyesha hatari wakati wowote na hasa kuanzia dakika ya 16 hadi 30 na 31 hadi 45 ambazo amefunga mabao matatu kwa kila kipindi, maana yake sita.
Bado kuna nafasi kwa kina Aguero na Kane, kwa kuwa nafasi ya kufunga wanayo lakini hii inaonyesha lazima wabadilike, kama milango bado si rafiki sana wanapokuwa wanacheza nyumbani, basi waongeze nguvu ya kuwa msaada katika timu zao kwa mechi za ugenini.


   

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic