January 7, 2020


BAO la umbali wa mita 18 alilolifunga kiungo wa Yanga, Mapinduzi Balama katika dakika ya 49, limemtia ubaya kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula.

Balama alifunga bao hilo wakati timu hizo zilipovaana katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya kumnyang’anya kiungo wa Simba, Mzamiru Yassin kabla ya kuukokota kidogo mpira na kupiga shuti kali.

Katika mchezo huo uliojaa upinzani mkubwa, mabao ya Simba yalifungwa na Meddie Kagere kabla ya Deo Kanda kuongeza la pili huku yale ya Yanga yakipachikwa na Mapinduzi Balama pamoja na Issa Mohamed ‘Banka’.

Mara baada ya bao hilo kuingia wavuni, mashabiki wa Simba walionekana kuchukizwa wakidai ndiyo aina ya mabao ambayo kipa huyo anaichezea Taifa Stars anafungwa kila wakati.

Mashabiki hao walisikika wakimtaka kipa namba mbili Beno Kakolanya kuwa ndiye aanze kuaminika na awe kipa namba moja kutokana na kiwango chake ambacho amekuwa akionyesha kila siku.

Haikuishia hapo, mashabiki hao walionekana wakizagaa uwanjani hapo wakimjadili Manula huku wakiendelea kusisitiza Kakolanya ndiye awe kipa namba moja.

“Tumechoshwa na aina ya mabao ambayo Manula amekuwa akifungwa kwenye baadhi ya mechi ambazo tumezicheza kati ya hayo, mengi ni ya mashuti ya umbali mkubwa kuanzia 18 na 20.

“Anaonekana kushindwa kuicheza kabisa mipira inayopigwa umbali mkubwa, hivyo kama anashindwa kucheza mipira hiyo hakuna sababu ya kuendelea kumtumia na badala yake atumiwe Kakolanya mwenye uwezo wa kudaka mipira hiyo,” alisikika shabiki wa Simba.

Championi Jumatatu, juzi lilimtafuta Manula kuzungumzia hilo, hakuwa tayari kutoa ushirikiano akidai yupo safari anaelekea Pemba kujiandaa na Kombe la Mapinduzi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic