January 1, 2020


WAKATI Ligi Kuu Soka Tanzania Bara ikiendelea kutimua vumbi kwenye viwanja mbalimbali nchini, Championi Jumatatu linakuletea baadhi ya wachezaji ambao wanafanya makubwa kwenye timu zao lakini hawatajwi sana midomoni mwa mashabiki na wapenzi wa soka nchini.

Kwa kiasi kikubwa wachezaji hawa wamekuwa na msaada chanya katika kuhakikisha timu zao zinapata alama tatu, au ushindi kwenye michezo husika wanayocheza. Kwa kiasi kikubwa wachezaji hawa wamekuwa na mchango mkubwa kwenye timu zao lakini hawana nyota ya kuimbwa midomoni mwa mashabiki wa timu zao.

MZAMIRU YASSIN; kiungo mkabaji wa Simba ambaye kazi yake anayofanya uwanjani hakuna mtu asiyeijua, ni kiungo anayekupa kila kitu unachohitaji, kuanzia kukaba hadi kusukuma mashambulizi kwenye lango la timu pinzani, Mzamiru licha ya umahiri wake uwanjani lakini amekuwa hatajwi sana midomoni mwa mashabiki wa Simba na hata anapokosekana husikii wakilalamika kama ilivyo kwa wachezaji wengine.

DEUS KASEKE; ni kiungo mshambuliaji anayekipiga kwenye kikosi cha mabingwa wa kihistoria Yanga SC, Kaseke pia anaingia kwenye kundi la wachezaji ambao kwa kiasi kikubwa wanafanya makubwa uwanjani lakini hawana bahati ya kuimbwa midomoni ma mashabiki wa Yanga, utasikia akisifiwa Sibomana au David Molinga wanaopachika mabao lakini kazi kubwa inakuwa imefanywa na akina Kaseke, kuna kipindi hadi baadhi ya mashabiki wapenda chenga na kanzu hupiga kelele kwa mwalimu amfanyie mabadiliko kwani hawaelewi anachokifanya uwanjani.


LAURIAN MPALILE; nahodha wa kikosi cha Tanzania Prisons anaingia kwenye orodha hii pia, Laurian anahudumu kwenye nafasi ya mlinzi wa kushoto na amekuwa mhimili mkubwa wa kikosi cha Tanzania Prisons ambacho hadi sasa kimepoteza mchezo mmoja tu wa Ligi Kuu Tanzania Bara huku kikiwa nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi kuu, ndani ya kikosi cha Wajelajela wanaotajwa sana ni akina Ismail Aziz, Cleophace Mkandala na akina Salum Kimenya.

GERSON FRAGA; labda kwa sababu hapigi chenga wala kumpiga mtu kanzu, hii inaweza kuwa miongoni mwa sababu ambazo zinafanya kiungo huyu wa Kibrazil asitajwe sana midomoni mwa mashabiki wa Simba, kwa kiasi kikubwa Gerson Fraga amekuwa msaada mkubwa kwenye safu ya kiungo ya Simba hasa anapokosekana Jonas Mkude na wakati mwingine Mzamiru Yassin, ana uwezo mkubwa wa kuzuia mashambulizi ya timu pinzani kwa ustadi mkubwa na kuifanya safu ya ulinzi ya Simba kuwa salama kwa kipindi chote cha mchezo.

MWADINI ALLY; tangu ajiunge na mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Azam FC mwaka 2015, Mwadini ameonekana kama mchezaji wa kawaida sana ndani ya Azam licha ya makubwa ambayo ameshayafanya hadi sasa, magolikipa wengi wamepita kwenye kikosi cha Azam kama Aishi Manula, Deo Munishi na sasa Razack Abarola lakini mkongwe huyu ameendelea kupambana ndani ya kikosi hicho licha ya kukosa nafasi mara kwa mara, ikumbukwe kwamba Mwadini Ally aliibuka shujaa kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho uliozikutanisha Azam FC na African Lyon ambapo alifanikiwa kucheza penalti moja na kuifanya Azam isonge kwenye hatua inayofuata ya mashindano hayo.

BRUCE KANGWA; miongoni mwa mihimili mikubwa kwenye safu ya ulinzi ya Azam FC ni Bruce Kangwa, si suala la ulinzi tu Kangwa anapandisha timu na kusaidia mashambulizi kwenye lango la timu pinzani lakini amekuwa hana nyota ya kuimbwa sana na mashabiki wa timu hiyo na kwa kiasi kikubwa utasikia akitajwa Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Frank Domayo au Richard Djodi.

TAIRONE SANTOS; kwa kiasi kikubwa amefanikiwa kuingia kwenye mfumo wa Simba SC, huku akiendelea kuwapa wakati mgumu Yusuph Mlipili na Kenedy Juma, Tairone alikuwa miongoni mwa wachezaji wa kigeni ambao usajili wao ulibezwa sana lakini hivi sasa amekuwa mhimili mkubwa kwenye safu ya ulinzi ya Simba SC akisaidiana na Pascal Wawa na wakati mwingine Erasto Nyoni, licha ya mchango mkubwa aliouonyesha kwenye kikosi cha Simba, bado Tairone amekuwa hatajwi sana kama ilivyo kwa wachezaji wengine wa kikosi hicho cha mabingwa wa nchi.


1 COMMENTS:

  1. Kwa kifupi tu Simba wapo vizuri hivi sasa wana idadi kubwa ya wachezaji wenye uwezo na wakiendelea katika hali ya utulivu hivi hivi basi wanaweza kufanya makubwa Africa.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic