KITENDO cha kuamini imemaliza mchezo na wachezaji wa Mtibwa Sugar kufuata maelekezo vema, ndicho kilichoisaidia kupata bao la 'usiku' la kusawazisha na hatimaye kushinda kwa changamoto ya mikwaju ya penalti dhidi ya Yanga juzi, kwa mujibu wa kocha Zuberi Katwila.
Katika mechi hiyo ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi iliyopigwa Uwanja wa Amaan, Yanga ilipata bao la kuongoza katika dakika ya 36 kupitia kwa Deus Kaseke.
Bao hilo lilidumu hadi dakika ya 90 kabla ya Shomari Kibwana kusawazisha na hatimaye mikwaju ya penalti kuchukua hatua yake na Mtibwa Sugar kushinda kwa matuta 4-2, hivyo kutangulia fainali.
Kocha wa Mtibwa Sugar, Katwila, alisema wangeweza kumaliza mchezo huo mapema, lakini wachezaji wake walishindwa kutumia nafasi nyingi walizopata.
Alisema kilichoigharimu Yanga zaidi ni kuamini wamemaliza mchezo na kutopambana kwa dakika zote 90.
Aidha, kuelekea mechi ya fainali Jumatatu ijayo, Katwila alisema kikosi chake kipo tayari kuvaana na timu yoyote iwe Azam au Simba.
"Unapoingia fainali utakuwa tayari kucheza na yeyote, kama ukiniuliza ni chague, basi nitakwambia nisikutane na yeyote," alisema.
Katika mechi hiyo ya juzi, Kipa wa Yanga, Ramadhani Kabwili alipangua penalti ya kiungo Abdulhalim Humud, hata hivyo, beki Kelvin Yondani aligongesha mwamba na kiungo Abdulaziz Makame akapaisha juu ya lango.
Wafungaji wa penalti za Mtibwa Sugar walikuwa ni Omary Sultan, Dickson Job, Jaffary Kibaya na Shomari Kibwana na zile za Yanga zilifungwa na Paul Godfrey ‘Boxer’ na kiungo Mapinduzi Balama.
CHANZO: RADIO ONE
0 COMMENTS:
Post a Comment