Licha ya kukerwa na matokeo ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Yanga, kocha mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Sven Vandenbroeck amefurahishwa na kasi na pasi za kiungo mpya wa timu hiyo, Luis Miquissone, raia Msumbiji.
Miquissone amejiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambayo ilimtoa kwa mkopo kwenda Klabu ya UD do Songo ya Msumbiji.
Vandenbroeck ameonekana kuvutiwa na kiungo huyo kutokana na uwezo aliouonyesha kwenye mazoezi ya timu hiyo tangu alipotua Alhamisi ya wiki iliyopita.
Taarifa kutoka ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo, zinasema kuwa Mbelgiji huyo amevutiwa na kiungo huyo mwenye uwezo wa kucheza kama winga kutokana na kasi yake pamoja pasi za uhakika.
“Kiukweli mwalimu ameonyesha kuvutiwa na Miquissone kutokana na kazi kubwa anayoonyesha ndani ya muda mchache na anaonekana kuzoea mazingira kuingia kwenye mfumo haraka sana.
“Mwalimu mwenyewe amekuwa anasema atakuwa msaada kutokana na kasi kubwa ya kuweza kuingia na mpira lakini hata pasi zake anaamini zitaisaidia timu hiyo,” alisema mtoa taarifa.
0 COMMENTS:
Post a Comment