January 18, 2020


KATIKA kipindi cha siku 30 zilizopita Yanga wameitengeneza sura mpya ya kikosi chao baada ya kufanya usajili kabambe kwenye dirisha dogo la usajili. Kwanza walisajili wachezaji ambao wameongeza nguvu katika kikosi hicho kisha wakaleta sura mbili za watu wapya wa benchi la ufundi.

Watu hao ni Mbelgiji Luc Eymael, ambaye amekuja kuchukua nafasi ya ukocha mkuu katika klabu hiyo na Riedoh Berdien, raia wa Afrika Kusini anayetua kubeba mikoba ya kocha wa fitinesi na kocha msaidizi wa pili.

Baada ya watu hao wawili kutua sasa kunalifanya benchi la ufundi la Yanga kuwa na makocha watatu, Eymael, Berdien na Charles Mkwasa. Eymael ambaye ametua nchini Alhamisi iliyopita amezungumza na Championi Juamatano, juu ya mipango yake mbalimbali baada ya kutua klabuni hapo na anafunguka kama ifuatavyo.

“Kwanza najua Yanga ni timu kubwa kwa hapa Tanzania, unaweza kuifananisha na timu kubwa nyingine za Afrika. Najua kile ambacho wanakitaka,” anaanza kusema Eymael.

NINI ULICHUKUA KATIKA MECHI ILE YA MAPINDUZI?

“Niliangalia mechi ile lakini nilichukua vitu vichache ambavyo nitavifanyia kazi kwa kuchambua baadhi ya vitu ambavyo naona vitanifaa.



UMETUA SASA, KIPI UTAFANYA CHA KWANZA?

“Nilikuwa kule Zanzibar ambapo niliitazama timu katika Mapinduzi Cup, lakini hiyo haitoshi nitahitaji muda zaidi wa kuangalia wachezaji wangu.

“Nitawaangalia wachezaji kwa siku saba ambazo naamini nitapata mwanga wa nini ambacho ninakitaka kutoka kwao na baada ya hapo nitasema nini cha kufanya.

UTABADILISHA CHOCHOTE KIUFUNDI?

“Hapana huwezi kubadili kila kitu haraka hivyo, inapasa kutenga muda kujua kila kitu. Sijui nini kitatokea kama nitabadili mambo ya kiufundi, lakini tunaweza kubadili namna ya kufanya mazoezi ambapo inawezekana kufanya jioni lakini nalo tunahitaji kusubiri.

ULIIJUA YANGA KABLA YA KUJA?

“Ndiyo nilikuwa naijua kwa sababu nilikuwa naifuatilia. Kumbuka nilikuwa Rayon Sports ya Rwanda, kwa hiyo nilikuwa naijua lakini pia naijua Ligi ya Tanzania kwa sababu nilikuwa naifuatilia japo siyo sana.

NINI UNAONA KITAKUBEBA HAPA YANGA?

“Nimekuja Afrika tangu mwaka 2010, nina miaka 10 hapa tangu wakati ambao nilifika mara ya kwanza. Kwa hiyo nina uzoefu wa hali ya juu ambao ndiyo utakaonibeba katika klabu yangu hii mpya.

UMEJIWEKEA MALENGO GANI HAPA?

“Kitu cha kwanza ni kugombea nafasi tatu za juu kisha tutafute nafasi ya kutwaa ubingwa kwa ajili ya kufuzu michuano ya kimataifa iliyo chini ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf). Lakini katika hilo Mungu ndiye anajua.

“Lakini pia nataka kuirudisha timu katika enzi za makombe kama ilivyokuwa huko nyuma, hayo ndiyo malengo yangu kwa kipindi hiki.

“Ila ijulikane mimi nafundisha na wachezaji wao ndiyo wanacheza, kwa hiyo nahitaji sana wachezaji wajitume kufikia haya ambayo ninayataka. Nitajitahidi kwa uwezo wangu kuifanya timu bora na ya ushindani.

UNAONA MECHI ZENU ZITAKUWA VIPI?

“Ujue mechi ni kama vile mtihani kwa wanafunzi wa shule, baada ya kufundishana kwa wiki nzima. Sijui itakuwaje lakini kitu cha msingi ni kuonyesha juhudi na kutaka kupata kitu kile kilicho bora.

UNAHOFIA KUCHEZA NA SIMBA?

“Kocha ambaye amefundisha timu kubwa kama AS Vita na akacheza na TP Mazembe lakini pia akafundisha timu kama Al-Merrikh SC na akafundisha Afrika Kusini ambapo kuna timu za Orlando Pirates na Kaizer Chiefs anaogopaje kucheza na Simba?

“Siwezi kuwaogopa kwa sababu nina uzoefu na mechi za dabi, japokuwa naelewa jinsi mechi hizo namna zinavyokuwa. Najua kabisa hiyo mechi na Simba ni kubwa kwa Afrika ambapo unaweza kuifananisha na Zamalek na Al Ahly au TP Mazembe na AS Vita.

“Nafurahia sana mechi za namna hiyo na sina kabisa hofu nazo, lakini pia nilifuatilia ile mechi ya 2-2, haikuwa kitu kidogo kutoka nyuma kisha kuja kurudisha mabao yote yale, niwapongeze kwa hilo na mwisho ieleweke mnapokuwa uwanjani katika zile dakika 90 kila timu inakuwa na asilimia 50 za kushinda.

UMEJIANDAAJE NA MATOKEO MABAYA?

“Siyo kitu kizuri sana lakini inabidi watu wajue kwamba soka lina matokeo matatu. Utafungwa, utapata sare na utashinda lakini sitarajii sana kuona tunapata matokeo mabaya.

“Tutashirikiana na wachezaji wangu kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri katika mechi zetu,” anamaliza Eymael.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic