MASHABIKI wa Simba kwa sasa wanaumia kwa kile ambacho wamekipata baada ya timu yao kupoteza mbele ya Yanga kwenye mchezo uliochezwa Machi 8, Uwanja wa Taifa majira ya saa 11:00 jioni.
Simba ambao waliingia uwanjani wakiwa na imani ya kufanya vizuri walikuwa na haki ya kufanya hivyo kutokana na ukweli kwamba kila mmoja anaamini kile anachokifikiria lakini mwisho wa siku mwamuzi wa yote anakuwa ni dakika 90.
Tuliona namna walivyokuwa na tambo kuhusu upana wa kikosi chao licha ya kufanya usajili makini ila bado kuna kazi ilitakiwa kufanya kufikia malengo ambayo walijiwekea mwanzo wa msimu.
Kufikia mafanikio kunahitaji juhudi isiyo ya kawaida kwa timu zote ili kuongeza wepesi katika kazi ambayo wanaifanya wachezaji ndani ya uwanja na nje ya uwanja.
Tunaona kwamba kila timu iliingia uwanjani na mbinu zao makini kwa lengo la kupata matokeo na mwisho wa siku Yanga ikasepa na pointi tatu muhimu wanastahili pongezi kwa kuwa walistahili na walionyesha nia ya kupambana kwa kile ambacho walikuwa wanakihitaji.
Kazi kubwa ambayo imefanywa na wachezaji wa Simba inapaswa ipewe pongezi pia kwa kuwa walicheza kwa juhudi kutafuta matokeo na mwisho wa siku wakapata kile amacho walikistahili baada ya dakika tisini kukamilika.
Yanga wameweza kupata walichokipanda wanastahili pia pongezi huku wale wa Simba nao wakistahili pongezi kwa kucheza mpira mzuri licha ya kushindwa kupata matokeo.
Mpira una matokeo matatu ambayo ni kushinda, kufungwa na kutoka sare yote ni matokeo ya mpira ambayo yanapaswa yapokelewe na mashabiki pamoja na hayo anayepata ushindi ni Yule aliyejipanga.
Tunaona kuna tabia za mashabiki kubeba matokeo mfukoni ambazo zilikuwa zinatawala kwenye mechi za hivi karibuni lakini Machi 8 kidogo walianza kuelewa kwamba mpira una matokeo matatu na wachache walikuwa na matokeo yao mfukoni.
Kikubwa ambacho kinatakiwa kichukuliwe na kiwe ni mwendelezo kwa mashabiki ni kupokea matokeo kwa mikono miwili na kuendeleza ushirikiano uliokuwepo awali kwani kufungwa na Yanga sio jambo geni kwenye maisha ya soka ni vitu ambavyo vipo kama ambavyo Simba imekuwa ikimfunga Yanga pia.
Kuna mashabiki ambao wamekuwa wakiweka ahadi ngumu ambazo kuzitekeleza kwakwe kunahitaji kujitoa hili pia kwa mashabiki wana kazi ya kulifanyia kazi kabla hawajaingia kwenye matatizo.
Mashabiki wanatakiwa kujiwekea mipaka na kuamini kwamba kwenye mechi hakuna timu ya kuibeza hata iwe namna gani kwani kudunda kwa mpira kuna mengi ambayo yanatokea kuna wakati timu inakuwa bora ila inashindwa kupata matokeo kutokana na namna ambavyo wachezaji wameshindwa kujitoa kwa kudharau mechi ama mpango wa mwalimu kuwa mgumu kwao kupata matokeo.
Tunaona wachezaji wa Yanga namna walivyoanza kwa kushambulia mwanzo wa kipindi jambo lililowapa hali ya kujiamini wachezaji wote huku wale wa Simba wakianza kuingia na hofu licha ya ubora wa kikosi walichonacho.
Lamine Moro, beki kisiki wa Yanga amefanya kazi kubwa na kuwaonyesha kwamba waliombeza awali hana uwezo hawakuwa sawa kwani alifanya kazi kubwa ndani ya uwanja na kuifanya ngome yao kuwa salama.
Ilikuwa ngumu kwa Simba kuitoboa ngome ya Yanga kutokana na ukuta uliokuwa umewekwa pamoja na ile hamasa kwa wachezaji namna ilivyokuwa na mwisho wa siku matokeo yakapatikana.
Mzigo mkubwa unakuwa kwa Simba ambao wanaona kwamba walistahili kushinda ila wamepoteza kutokana na uzembe wa wachezaji wao hili liliwagharimu kwenye mchezo wa kwanza ambao ulichezwa Januari 4 limewatafuna tena kwenye mechi ya pili.
Kuna suala la kujifunza hasa kwa wachezaji wazawa na wageni namna ambavyo wanajituma ndani ya uwanja na kufanya kazi zao kwa kujiamini jambo ambalo linawafanya wawe bora.
Mzamiru Yassin juhudi zake zote kwa sasa zimesahaulika huku akibaki Jonas Mkude peke yake katikati jambo linaloongeza ugumu katika kutafuta matokeo.
Tukiachana na matokeo bado kuna suala la wachezaji kushindwa kulinda wachezaji wenzake ndani ya uwanja kwa kucheza bila kuwajali.
Tumeona nyota wa Simba, Clatous Chama alionekana akimchezea rafu dhahiri kabisa kiungo wa Yanga, Feisal Salim ‘Fei Toto’ jambo ambalo si la kiuungwana.
Wachezaji hawa wanapaswa wafundishwe adabu kwanza na klabu zao kabla ya mamlaka husika ambazo ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hawajafanya maamuzi yao.
Labda ingekuwa ni rahisi kwa wachezaji wote kucheza kwa nidhamu kwa kuwa kuna presha kutoka ndani ya uongozi wa timu pia kuna presha kutoka ndani ya uongozi itasaidia kuwapa presha pia wakiwa ndani ya uwanja.
0 COMMENTS:
Post a Comment