NIMESIKIA kuna
mpango wa kuzitaka timu za ligi kuu kuwa na timu za vijana chini ya miaka 15.
Ni wazo zuri
ambalo litasaidia sana kuzalisha wachezaji ambao watakuwa faida kubwa kwa siku
za baadae.
Wenzetu wote
walioendelea waliwekeza kwenye soka la vijana na leo hii wanaringa na mafanikio
yao.
Wenzetu
walianza kitambo sana na walijua nini faida ndio maana leo wanakula matunda
yake tena kwa raha kubwa.
Sisi kama
tutakuwa makini na mpango huo nina hakika tutafanikiwa tena sio siku nyingi
ndani ya miaka mitano tu au mbele kidogo.
Tatizo langu
ni kwamba je tutaweza kulisimamia suala hilo ambalo ni kubwa mno sio la
mchezomchezo.
Nasema hivyo
kutokana na jinsi historia ilivyo kwenye soka letu ambalo tunaanzisha mambo
mengi ila kuyaendeleza ni tatizo.
Nakumbuka
kuna kanuni ya ligi kuu inayoziamuru timu zote za ligi kuu kuwa na timu za
vijana za chini ya miaka 20, lakini utekelezaji wake wote tunaujua.
Timu nyingi
za ligi kuu hazina timu imara za hao vijana na hata hao TFF wanajua sasa
wanakuja na huo mpango wa chini ya miaka 15.
Kikubwa ni
kwamba timu zetu nyingi za ligi kuu hadi daraja la kwanza zina hali mbaya
kiuchumi na haziwezi kuziendesha hizo timu za vijana chini ya miaka 20, sasa
zitaweza kuendesha timu za miaka 15?
Hapa kuna
matatizo mawili ya kiuchumi na uelewa hasa kwa hao viongozi wa timu ambao sijui
kama watalipokea kwa umakini unaotakiwa.
Nilipomsikia
Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Oscar Mirambo analielezea suala hilo nilijawa na
maswali mengi lakini acha niseme kweli nimelipenda wazo lake na lina faida kwa
soka la nchi hii, lakini tatizo ni mfumo wetu.
Uwekezaji ni
mdogo mno kwenye soka letu ambalo hadi leo hatujui thamani halisi ya ligi yetu
na wengi wanashindwa kulijibu swali hilo kwa sababu wanajua mateso yanayotokea
kwenye klabu.
Wenzetu soka
ni biashara kubwa tena yenye kuingiza mamilioni ya fedha ndio maana wanafanya
wanavyotaka ila kwetu ni tatizo kwa sababu timu zetu ni maskini na hazina pesa
kabisa.
Klabu nyingi
za Bongo zinalia njaa, hali ni ngumu kwao na sasa hao watu wanapewa mzigo wa timu
za chini ya miaka 15 sijui kama wataweza kuubeba.
Sidhani kama
ulifanyika uchunguzi wa namna klabu zetu zilivyo, kisha ndiyo kuja na suala
hilo la kuwa na timu za chini ya miaka 15.
Kama
nilivyoeleza hapo awali, hivi sasa timu za ligi kuu zina timu za vijana chini
ya miaka 20, zamani kulikuwa na mpango wa kila timu ikienda kucheza mechi ya
ligi, basi zitaanza kupambana timu zao za vijana, ndipo wakubwa wanafuata.
Lakini mara
kadhaa tumeshuhudia pale Uwanja wa Taifa jijini Dar, Simba ikiwa inacheza na
Mbao, basi vijana wa Simba wanatafutiwa timu yoyote kucheza nayo, kisha ndiyo
wakubwa wanafuata, na wakati mwingine hakuna kabisa hizo mechi za vijana.
Kinachopendeza
ni kwamba, siku ya mechi ya watani, Simba dhidi ya Yanga, ndiyo huwa
tunashuhudia mengi, vijana wao wanaanza kukipiga, kisha wakubwa wanafuata.
Sasa huu
mpango wa sasa wa kuwa na timu za vijana chini ya miaka 15 ulifanyiwa uchunguzi
kabla au kupeana mizigo tu.







0 COMMENTS:
Post a Comment