BAADA ya kufanikiwa kufuta ukame wa miezi sita bila kufunga bao lolote ndani ya Yanga, mshambuliaji wa klabu hiyo, Yikpe Gislain Gnamien, amefunguka kilichokuwa nyuma ya pazia.
Yikpe amesema alikuwa anashindwa kufanya vizuri ndani ya timu hiyo kwa sababu alikuwa ametawaliwa na presha ya ndani na nje ya uwanja, kiasi ambacho alikuwa anashindwa kurejea kwenye ubora wake kila mara alipokuwa anapata nafasi ya kucheza.
Mara ya mwisho Yikpe kufunga bao ilikuwa ni Januari 26 kwenye mchezo wa FA, Yanga wakiwachapa Tanzania Prisons kwa mabao 2-0, siku ambayo Bernard Morrison alitikisa nchi kwa kupanda juu ya mpira.
Yikpe alifuta ukame huo wa kutofunga ndani ya Yanga baada ya Julai 15, Jumatano kufanikiwa kufunga bao moja, wakati Yanga wakiwachapa ‘vibonde’ Singida United kwa mabao 3-1.
Hiyo inakuwa mara ya pili kwa Yikpe kuwafunga Singida msimu huu, kwani katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Liti, alifunga bao moja Yanga wakishinda 3-1.
Yikpe amesema: “Nilikuwa na presha sana kiukweli, kukaa bila kufunga kwenye timu kubwa kama Yanga kwa mshambuliaji kama mimi inakuwa mbaya sana, presha ilikuwa ndani na nje ya uwanja kwa upande wangu, nilikuwa nashindwa kurudi kwenye fomu yangu kwa sababu ya presha.
“Nafurahi sana kiukweli kufanikiwa kufunga bao baada ya muda mrefu, siwezi kuelezea namna ambavyo najisikia furaha kwa kuweza kufunga tena baada ya kipindi kirefu kupita, naamini kuwa hii inakwenda kunirejesha tena mchezoni. Nafurahi sana,” alisema Yikpe.
Yanga leo ina kibarua cha kumenyana na Mwadui FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa Uwanja wa Taifa.
0 COMMENTS:
Post a Comment