August 18, 2020

 

MAKAMU wa Rais,  Samia Suluhu,  ameikabidhi Kampuni ya Global Publishers Tuzo kutoka Benki ya CRDB Agosti 16, 2020, ikiwa ni shukrani ya kuthamini mchango wa kampuni hiyo katika mashindano ya mbio za CRDB Bank Marathon zilizolenga kuhamasisha uchangiaji wa shilingi milioni 200 za kusaidia gharama za matibabu kwa watoto 100 wenye uhitaji wa upasuaji wa moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Muhimbili.

 

Akizungumza na Global Digital, Mhariri Mtendaji wa Global Publishers, Saleh Ally ‘Jembe’, amesema kuwa anaishukuru CRDB kwa tuzo hiyo kwani ni heshima kubwa kwa kampuni yake huku akiahidi kuwa Global itaendedelea kushiriki katika shughuli zote za kijamii, kuziunga mkono taasisi zenye nia ya dhati ya kuwasaidia Watanzania pamoja na kuunga mkono jitihada za Serikali katika sekta mbalimbali.

 

“Kwa niaba ya kampuni ya Global Publishers ambayo ni sehemu ya Global Group tunasema ni jambo zuri sana, hii Tuzo ilikuwa ni kusapoti CRDB Marathon 2020, ambapo mashindano haya ya riadha yalikuwa yamegawanyika katika vipengele mbalimbali.

 

“Kwanza kulikuwa kuna baiskeli, kulikuwa kuna riadha kwa maana ya kukimbia tu, pia kulikuwa na vipengele vingine vya kilometa 21, 42, 5, 10 na ya mwisho kabisa walikuwa wametembea viongozi kama uliona Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na mke wake Mama Salma Kikwete, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan naye alikuwepo na ndiye aliyetukabidhi Tuzo hii, kuonyesha ni kiasi gani tunasapoti michezo.


“Tulisapoti michezo hii kupitia magazeti ya michezo ya Championi na Spoti Xtra lakini pia katika Global TV na Global Digital kwa ujumla, pia tulikuwa kama sehemu ya wadhamini wa mbio hizi, tulifanya kazi ya kuitangaza na kuwavutia watu na kama ulifuatilia utaona tiketi au watu kujisajili kwa kilometa tano ziliisha ndani ya siku mbili tu baada ya kuwa tumetangaza.

 

“Baadaye wakalazimika kutangaza tena kuwaambia watu kwamba mambo yanaendelea, wakarudisha zile kilometa tano  ambapo watu waliongezeka zaidi na kwa kweli zilifana sana na hata wao CRDB walikuwa wamejiandaa sana. Kwa hiyo sisi tumepata faraja sana  kwa sababu tunaamini wapo wengine hawakuweza kuliona hili wala kulithamini.

 

“Lakini tunaamini mara nyingine watajitokeza kwa wingi zaidi na tuwashukuru CRDB walituonyesha ushirikiano mzuri sana. Labda niwashauri tu kwamba hii isiwe mwisho waendelee namna hii, kwa sababu mwisho wa siku hii ni burudani  lakini ni kwa ajili ya afya na inawakutanisha watu wa rika mbalimbali, kujadili mambo mbalimbali, naamini kabisa mpaka siku hii riadha imefika mwisho kuna watu watakuwa wamefahamiana kibiashara na hii naichukulia kama ni sehemu ya kujenga taifa letu," amesema.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic