MAANDALIZI kuelekea mbio za wazi za Mount Hanang' Marathon yameendelea kupamba moto katika mikoa ya Arusha, Manyara na Singida huku mbio hizo zikitarajiwa kufanyika kesho mjini Katesh.
Mbio hizo za wazi za kilomita 21, kilomita 10 na kilomita 5 zitafanyika Katesh wilayani Hanang' Mkoa wa Manyara, zinatarajiwa kushirikisha zaidi ya wanariadha 1,000 kutoka ndani na nje ya nchi. Mbio hizo zimeandaliwa na taasisi ya Gidabuday Sports Tourism Foundation.
Mratibu wa mashindano hayo ambaye ni katibu mkuu wa zamani wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday alisema zoezi la usajili limeshika kasi katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Ofisi za Gidabuday Sports Tourism Foundation zilizopo Namfua Plaza Arusha, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Ofisi ya Mkurugenzi wa mji wa Babati na Ofisi ya Ofisa michezo mji wa Babati.
Gidabuday amewaomba wanariadha wote wanaotarajia kushiriki wafike kujiandikisha tayari kwa ajili ya kushiriki mbio hizo kesho ambapo gharama ya usajili ni Sh 15,000.
Alisema lengo la mbio hizo ni kutafuta vipaji vipya ili kuviendeleza, kuhamasisha amani kuelekea uchaguzi mkuu, kuandaa semina kwa waalimu wa michezo wa shule za msingi na sekondari na kuutambulisha umma wa Wanahanang’ juu ya mpango mkakati wa uwanja wa michezo wa kimataifa unaotarajiwa kujengwa Katesh kwa usimamizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang'.
0 COMMENTS:
Post a Comment