MZUNGUKO wa sita upo njiani kwa sasa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo unatarajiwa kuanza kutimua vumbi Oktoba 14.
Rekodi zote ambazo ziliwekwa ndani ya raundi nne zimegonga mwamba kuendelea kudumu na zimevunjwa kibabe ndani ya raundi ya tano.
Hapa tunazitazama zile rekodi ambazo ziligonga mwamba kudumu ndani ya ligi kuu baada ya raundi ya tano kuchezwa mambo yalikuwa namna hii:-
Yanga 3-0 Coastal Union
Ilikuwa ni mwendo wa mojamoja kwenye mechi zake nne za mzunguko wa nne ndani ya Ligi Kuu Bara wakati ilipokuwa chini ya Kocha Mkuu, Zlatiko Krmpotic.
Ilianza namna hii:-Yanga 1-1 Tanzania Prisons, Yanga 1-0 Mbeya City zilipigwa Uwanja wa Mkapa. Kisha Kagera Sugar 0-1 Yanga ilikuwa Uwanja wa Kaitaba na Mtibwa Sugar 0-1 Yanga Uwanja wa Jamhuri.
Mambo yalibadilika mzunguko wa tano, Oktoba 3 ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 mbele ya Coastal Union ambapo wote waliofunga waliweka rekodi kwa kufunga mabao yao kwa mara ya kwanza.
Carlos Carlinhos alifunga kwa kichwa bao lake la kwanza, Haruna Niyonzima alifunga kwa mguu la kushoto bao lake la kwanza na Yacouba Songne alifunga kwa mguu la kulia.
Mabao 20
Ilikuwa ni mwisho mabao 14 kufungwa ndani ya ligi na kuanzia mzunguko wa kwanza mpaka wa nne hakukuwa na mzunguko uliokusanya mabao zaidi ya 15.
Mzunguko wa kwanza yalifungwa mabao 13, mzunguko wa pili yalifungwa mabao 13, mzunguko wa tatu yalifungwa mabao 14 na mzunguko wa nne yalifungwa mabao 13.
Ngoma imepinduka mzunguko wa tano yamefungwa mabao 20 na kuvunja rekodi zote za mizunguko minne kwa kukusanya mabao mengi.
Azam FC 4-2 Kagera Sugar
Kwa mzunguko wa tano huu ni miongoni mwa mchezo bora na unastahili heshima yake kwa namna ambavyo timu zote mbili zilifunguka na kuwaacha wachezaji wacheze mpira.
Prince Dube wa Azam FC aliweza kudhihirisha kwamba yeye ni mwana wa mfalme kwa kuhusika kwenye mabao matatu kati ya manne ya Azam FC ambapo alifunga mabao mawili na kutoa pasi moja ya bao kwa Obrey Chirwa.
Ni mchezo ambao ulikusanya mabao mengi kuliko mechi zote ndani ya ligi kwa msimu wa 2020/21 ambayo ni jumla ya mabao sita.
Kissu kutunguliwa
Alicheza mechi nne ndani ya Azam FC bila kuonja joto ya kutunguliwa. Raundi ya tano aliokota 'visu' viwili langoni na kutibua rekodi yake kwenye mechi zilizopita.
David Luhunde hakuwa na huruma nje ya 18 kwa mguu wake wa kushoto kwa kupiga pigo huru lililomuacha huru David Kissu kwa mara ya kwanza kwenye ufalme wa kumiliki ‘clean sheet’.
Kisu cha pili alikutana nacho kutoka kwa mzawa mwenye ushikaji na nyavu, Yusuph Mhilu na kumfanya atunguliwe jumla ya mabao mawili ila timu yake ilisepa na pointi tatu.
KMC kupoteza nyumbani
Mechi mbili ilicheza Uwanja wa Uhuru na haikupoteza ilishinda mbele ya Mbeya City mabao 4-0 na mbele ya Tanzania Prisons ilishinda mabao 2-1.
Ilipoanza ziara nje ya Dar, ilishinda mbele ya Mwadui mabao 2-1 ngoma ilipinduka Kagera Sugar kwa kufungwa bao 1-0.
Ilichokutana nacho Uwanja wa Uhuru dakika ya 88 ilikuwa ni kichapo cha bao moja kutoka kwa Pius Buswita akimtungua kipa namba moja Juma Kaseja na kufanya ipoteze ufalme wa dakika 180 zilizodumu kwenye raundi zilizopita.
Gwambina kusepa na pointi tatu
Mambo yalikuwa ni magumu kwa Gwambina FC iliyopanda Ligi Kuu Bara ikitokea Ligi Daraja la Kwanza kwenye mechi zake nne za mwanzo.
Ilianza kwa kupoteza kwa kufungwa bao 1-0 mbele ya Biashara United, ililazimisha sare ya bila kufungana mbele ya Kagera Sugar ikaambulia kichapo cha bao 1-0 mbele ya Ruvu Shooting na kupokea kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Simba.
Ndani ya dakika 360 ilifungwa mabao matano huku safu yake ya ushambuliaji ikiwa haijafunga bao na iliibukia raundi ya tano kwa kushinda mabao 2-0 dhidi ya Ihefu mabao yote yakifungwa na Meshack Abrahm.
Mbeya City kuambulia pointi
Amri Said Kocha Mkuu wa Mbeya City anapitika kwenye wakati mgumu kwa sasa baada ya kikosi chake kucheza mechi tano mfululizo huku wakiwa hawajafunga bao hata moja.
Licha ya kupoteza kwenye raundi zake nne zilizopita raundi ya tano ilifanya kweli kwa kusepa na pointi moja mbele ya Tanzania Prisons kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
0 COMMENTS:
Post a Comment