HITIMANA Thiery, Kocha Mkuu wa timu ya Namungo amesema kuwa kwa sasa anafanyia kazi makosa ambayo wameyafanya kwenye mechi zao zilizopita ndani ya Ligi Kuu Bara.
Namungo imeanza kwa kasi ya kusuasua kwa msimu wa 2020/21 licha ya kushinda kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Septemba 6 kwa kuifunga Coastal Union bao 1-0.
Kwa sasa ipo kwenye maandalizi ya mchezo wake unaofuata ndani ya ligi dhidi ya Kagera Sugar utakaochezwa Oktoba 14, Uwanja wa Majaliwa.
Akizungumza na Saleh Jembe, Thiery amesema kuwa wanatambua wapo kwenye wakati mgumu kwa kupata matokeo ambayo hawayatarajii ila wanaamini watarejea kwenye ubora.
“Matokeo ambayo tunayapata kwa sasa hayafurahishi lakini hakuna namna zaidi ni kuangalia wapi ambapo tunakosea ili kuweza kuwa bora.
"Bado kuna mechi ambazo zipo mkononi mwetu na ni ngumu, tunachokifanya ni kufanyia kazi makosa ili kuweza kupata matokeo kwenye mechi zetu zijazo,” amesema.
Ikiwa imecheza mechi tano imeshinda mechi mbili na kupoteza mechi tatu ipo nafasi ya tisa na pointi zake sita kibindoni.
0 COMMENTS:
Post a Comment