CHRISTINA Mwagala, Ofisa Habari wa Klabu ya KMC amesema kuwa licha ya kupoteza kwa mechi zao mbili mfululizo kwenye ligi hawajatoka kwenye reli wataendelea kupambana kwenye mechi zao zijazo.
Mzunguko wa nne na wa tano ulikuwa mgumu kwa KMC baada ya kucheza mechi mbili mfululizo ndani ya ligi na kupoteza zote kwa kufungwa jumla ya mabao mawili.
Ilianza Septemba 25 kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar na ikapoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania, Uwanja wa Uhuru.
Kwenye mechi zote hizo mbili KMC ilifungwa na wachezaji ambao walikuwa wanaandika mabao yao ya kwanza ndani ya ligi, dhidi ya Kagera lilifungwa na Yusuph Mhilu na kwenye mchezo wao dhidi ya Polisi Tanzania ilifungwa 1-0 na Pius Buswita.
Christina amesema:"Tumepoteza mechi zetu mbili ambazo zimepita hilo lipo wazi lakini tunasema kwamba hayo yameshapita tunatazama yanayofuata mbele yetu kwani kuna mechi nyingi.
"Kupoteza nyumbani mbele ya mashabiki zetu inauma lakini hakuna namna ya kufanya zaidi ya kujipanga upya ili kuweza kupata matokeo kwenye mechi zetu zinazofuata. Mashabiki wasife moyo bado tupo imara," amesema.
Mchezo wao unaofuata ni dhidi ya Coastal Union ambayo imetoka kupoteza kwa kufungwa mabao 3-0 dhidi ya Yanga.
KMC ipo nafasi ya 7 ikiwa na pointi tisa baada ya kucheza mechi tano inakutana na Coastal Union iliyo nafasi ya 15 na pointi 4 nayo pia imecheza mechi tano.
0 COMMENTS:
Post a Comment