NYOTA wa Simba mwenye zali la kutupia kwenye kila mechi ndani ya Ligi Kuu Bara, Chris Mugalu ametengewa dakika 180 za kujiweka sawa kabla ya kuvaana na Tanzania Prisons kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuchezwa Oktoba 22.
Mugalu amefunga mabao matatu akiwa amecheza mechi tatu za ligi, alianza kufunga mbele ya Biashara United na alifunga mbele ya Gwambina FC zote zilichezwa Uwanja wa Mkapa kisha alifunga bao lake la tatu dhidi ya JKT Tanzania, Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Kwa sasa Simba imeandaa mechi mbili za kirafiki ikiwa ni mchezo dhidi ya Ndanda FC utakaopigwa Oktoba 13 na ule dhidi ya Mlandege FC ya Zanzibar ikiwa ni sehemu ya kukiandaa kikosi cha Simba kwenye mechi za ushindani na zote zitachezwa Uwanja wa Azam Complex.
Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara ameliambia Championi Jumatatu kuwa malengo ya mechi hizo ni kuwaandaa wachezaji wawe kwenye ubora katika mechi za ushindani zinazofuata.
“Tuna mechi nyingi za ligi kwa wakati huu kabla hatujazifikia benchi la ufundi limeona ni bora kuwa na mechi za kirafiki ambazo zitafanya kikosi kiwe na muunganiko mzuri ndani ya uwanja,” alisema.
0 COMMENTS:
Post a Comment