MATOKEO mabovu kwa msimu wa 2020/21 yanatajwa kuwa ni sababu ya Hitimana Thiery aliyekuwa Kocha Mkuu wa Klabu ya Namungo kufutwa kazi jumlajumla.
Ndani ya Namungo inayotumia Uwanja wa Majaliwa kwa msimu huu amekwama kuendelea ubora wake alioanza nao msimu uliopita wa 2019/20.
Hitimana awali aliweka wazi kuwa kwa msimu huu mambo yamekuwa magumu kutokana na ushindani ndani ya ligi kuongezeka pamoja na wachezaji wake kukosa muda wa maandalizi ya kutosha licha ya kwamba ilikuwa ni kwa dunia nzima kutokana na janga la Virusi vya Corona.
"Kweli kwa msimu huu wa 2020/21 tumeanza vibaya ni upepo mbaya ambao umetukumba ila sababu kubwa ni maandalizi mafupi pamoja na wachezaji kutokuwa na muunganiko mzuri," aliweka wazi kabla ya kufutwa kazi.
Jana Novemba 18, kupitia kwa Mwenyekiti wa Klabu ya Namungo, Hassan Zidadu ameweka wazi kuwa sababu ya kusitisha mkataba na kocha huyo ni mwendo mbovu wa timu hiyo.
"Tumefikia makubaliano ya kusitisha mkataba na Hitimana kwa kuwa timu haikuwa na mwendo mzuri kwenye matokeo ndani ya uwanja.
"Kwa sasa timu imeweka kambi Zanzibar na ipo chini ya Kocha Mkuu, Hemed Morocco," amesema.
Namungo ina kazi ya kuiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika na mchezo wake wa kwanza itakuwa dhidi ya Al Rabita ya Sudani Kusini Novemba 28, Uwanja wa Azam Complex.
Ikiwa imecheza mechi 10 ipo nafasi ya 9 na pointi zake kibindoni ni 14.
0 COMMENTS:
Post a Comment