JOSE Carlos Paz, atakayezichapa na Hassan Mwakinyo Novemba 13 kwenye ukumbi wa Next Door Arena Oysterbay amewasili na kutamba kutwaa ubingwa wa uzito wa Super Welter wa WBF unaoshikiriwa na Hassan Mwakinyo.
Bondia huyo raia wa Argentina amewasili na baba yake Alberto Ramon Paz ambaye pia ni kocha wake kama ilivyo kwa bondia Floyd Mayweather.
Akizungumza mara baada ya kuwasili, Paz amesema kuwa amesafiri umbali mrefu kwa ajili ya kutwaa ubingwa katika pambano hili linalojulikana kwa jina la Jackson Group Fight Night.
Paz amesema kuwa amechukua tahadhari kubwa kwa ajili ya Mwakinyo na kwamba siyo bondia mbaya.
“Nimefika mapema zaidi ili kuzoea hali ya hewa, hii ni moja ya mikakati ya ushindi, nilisafiri kwa basi na baadaye kupanda ndege, siku mbili nipo njiani, sitakuwa tayari kushindwa katika pambano hili,” amesema Paz.
Kocha wake, Alberto Ramon naye amesema kuwa wamemsoma Mwakinyo katika mapambano yake na kujua mbinu zake ambazo amezifanyia kazi.
“Tumefanya mazoezi magumu kuelekea pambano hili, tumefanya mazoezi ya ufundi na mbinu, hayo yote ni kwa ajili ya kusaka ushindi ambao tunaamini asilimia 100, tutashinda,” amesema Ramon.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jackson Group Sports, Kelvin Twissa amesema maandalizi yanaendelea vizuri na mabondia wa Zambia, Zimbabwe na Kenya watawasili wiki ijayo kwa ajili ya pambano hilo.
Twissa amesema kila kitu kiko katika hatua za mwisho na tiketi zitaanza kuuzwa kwa njia ya Nilipe na Selcom kwa Sh 3 Milioni kwa meza ya watu 10 na Sh150,000 kwa kwa viti vya kawaida.
Pambano hilo litatanguliwa na mapambano mengine matatu ambapo bondia nyota wa kike nchini, Zulfa Macho atazipiga na Alice Mbewe kutoka Zambia, Hussein Itaba atazichapa na Alex Kabangu wa DR Congo na Fatuma Zarika wa Kenya atacheza na Patience Mastara wa Zimbabwe.
0 COMMENTS:
Post a Comment