November 12, 2020

 


MZUNGUKO wa 10 umekamilika na kila kitu kimekwenda kwa namna ambavyo mipango ilikuwa ni jambo jema kuona kwamba kila kitu kimekuwa sawa.

Yale ambayo yametokea kwenye raundi hizi 10 ni muhimu kufanyiwa kazi ili kuweza kuleta mabadiliko kwa ajili ya wakati ujao hasa kwenye Ligi Kuu Bara ambayo imekuwa na ushindani mkubwa.

Matukio mengi ambayo yanatokea ndani ya uwanja yanawaumiza wale ambao wanatendewa vibaya kwa wakati huo lakini hawana chaguo kwa kuwa ikishaamuliwa imeamuliwa hakuna cha kufanya tena.

Mengi tumeshuhudia kwenye raundi 10 ambapo kila timu ndani ya ligi imekuwa ikionyesha ushindani hilo lipo wazi, pongezi kwa wachezaji pamoja na viongozi wa timu kwa namna ambavyo wanazidi kupambana.

Kila timu inaonekana imefanya maandalizi mazuri na wanaingia ndani ya uwanja wakiwa na imani ya kupata matokeo hilo ni jambo ambalo linapaswa liwe endelevu wakati wote ndani ya uwanja.

Wale ambao walikuwa wanamtindo wa kuingia ndani ya uwanja wakiwa na matokeo yao mfukoni matumaini yangu kuna jambo ambalo wamejifunza.


Mpira unadunda na dakika 90 hutoa matokeo sahihi ambayo wakati mwingine hutoa maumivu na muda mwingine furaha.

Tunaona kwamba taratibu kuna maboresho ambayo yameanza kuonekana na wachezaji nao wameanza kuonyesha kwamba mabadiliko hayo yana faida kwao hasa katika kusaka ushindi ndani ya uwanja.

Jambo la msingi kwa wakati huu ambao ligi imesimama timu kufanya tathimini na kuangalia pale ambapo zilikwama kupata matokeo ndani ya uwanja kwa raundi ambazo zimepita.

Ni wazi kwamba vita kubwa bado ipo ndani ya uwanja kwani raundi ya kwanza bado haijakamilika hivyo ni muhimu kupanga na kuchagua namna ambayo timu inaweza kufanya kwa ajili ya mechi zaijazo.

Mashabiki muda wote mnastahili pongezi kwa kuwa mnajitokeza kwa wingi viwanjani kuzipa sapoti timu zenu hili ni jambo jema wakati wote.

Uwepo wa mashabiki unaongeza hamasa na morali kwa wachezaji kupambana kufa na kupona kwenye kusaka matokeo ndani ya uwanja na inafurahisha pia kuona zile tambo nje na ndani ya uwanja.

Kila kitu ndani ya uwanja ni burudani, kuanzia uwepo wa mashabiki wachezaji wenyewe wote wanategemea sapoti pia kutoka kwa mashabiki hivyo ni muhimu kutambua kwamba uwepo wenu ni wa muhimu.

Msimu huu wa 2020/21 tunaona kwamba wapo baadhi ya mashabiki ambao walikumbwa na kasumba ya kufungiwa kujitokeza kushangilia timu zao.

Kwa hilo ambalo limetokea linapaswa kuwa somo kwa wengine kwa sasa kuziondoa tofauti zao na kuendelea kuishi wakiwa ni ndugu kwani timu zitabaki kuwa timu ila undugu na asili ya Tanzania ni amani na upendo.

Pongezi kubwa kwa wachezaji wa timu zote ambao wanapambana kwa wakati huu ni kuona kwamba wanaweza kufikia malengo ambayo wamejiwekea.

Mashabiki wengi wanazidi kujitokeza uwanjani na wameona ushindani na soka tamu ambalo wengi wanapenda kuliona siku zote hicho ndicho kikubwa tunachohitaji kwenye soka.

Kikubwa ambacho kinaonekana kwa sasa mashabiki wameanza kuonyesha ule uzalendo na upendo ambao ni asili ya Tanzania katika hilo pongezi pia mnastahili.

Zile tofauti zimeanza kuwekwa kando hilo ni jambo la msingi na inapaswa liendelee kukaa ndani ya mioyo ya mashabiki daima na milele na sio siku moja pekee.

Kwa kufanya hivyo kunawapa kazi wachezaji kuanzia ndani ya timu zao ambazo wanazitumikia kwa sasa pamoja na timu zao za taifa ambazo wameitwa kuzitumikia.

Jambo la msingi ni kuona kwamba kila mmoja anatimiza wajibu wake kuanzia kwa mashabiki na wachezaji ambao wamepewa majukumu kwenye timu zao za taifa.

Muda wote wachezaji mnapaswa kuwa makini na wapinzani wenu ili kulinda matokeo na pia katika kupata matokeo ni lazima kila mmoja atumie kosa la mpinzani kupata ushindi.

Kikubwa kwa sasa Watazania inabidi tukumbuke kwamba Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars ina kazi ya kufanya Novemba 13, nchini Tunisia kwenye mchezo wa kusaka tiketi ya kufuzu Afcon dhidi ya Tunisia.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Shirikisho la Soka Afrika, (Caf) ni kwamba mchezo huo utachezwa bila ya uwepo wa mashabiki kutokana na kuchukua tahadhari dhidi ya janga la Virusi vya Corona.


Hii ni timu ya kila mmoja anayeishi ndani ya Tanzania na nje ya Tanzania hivyo kazi yetu sisi ni moja kuipa sapoti kwa namna yoyote ile ili kuwapa deni wachezaji kutimiza majukumu yao ndani ya uwanja.

Ukiachana na timu ya Taifa ya Tanzania kuna Ligi Daraja la Kwanza ambayo nayo pia inakuwa kama imesahaulika hivi huku nako pia tuwekeze nguvu zetu bila kuchoka.

Timu ambazo zinapanda ndani ya Ligi Kuu Bara huku zinatengenezwa na mazingira yao yanaanzia huku ni muhimu kuyatazama mazingira yao ili kuwapa fursa ya kuleta ushindani pale watakapopanda.

Kwa timu ambazo zimekuwa na mwenendo mbovu benchi la ufundi lifanye kazi ya kurekebisha makosa na kutumia mbinu mpya kupata matokeo.

Wakati wa kufanya hayo mabadiliko ni sasa na mashabiki pia sapoti yenu ndani ya uwanja ni muhimu kwa kuzipa sapoti pia timu za Ligi Daraja la Kwanza kutatoa ushindani wa kweli mwanzo mwisho.

 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic