MAURICIO Pochettino, aliyekuwa Kocha Mkuu wa Tottenham kwa sasa anahusishwa kujiunga na Klabu ya Athletic Bilbao ili kubeba mikoba ya kocha Gaizko Garitano ambaye anapata tabu ndani ya La Liga kwa sasa akiwa ameongoza timu hiyo kucheza mechi nane na imekusanya pointi nane.
Uwezo wa wachezaji pamoja na benchi la ufundi vimekuwa vikiwapa mashaka mabosi wa timu hiyo jambo linalowafanya wafikirie kufanya mazungumzo na Pochettino raia wa Argentina ambaye kwa sasa hana timu.
Mbali na Pochettino wengine ambao wanatajwa kuwa kwenye hesabu za mabosi wa timu hiyo ni pamoja na kocha wa zamani wa Klabu ya Barcelona Ernesto Valverde ili wainoe timu hiyo.
Ishu kubwa ambayo imeripotiwa kuwa tatizo kumpata Muargentina huyo ni mkwanja mrefu ambao anautaka kocha huyo na inaelezwa kuwa Manchester United inayoshiriki Ligi Kuu England imefanya mazungumzo naye ili akainoe timu hiyo iliyo chini ya Kocha Mkuu, Ole Gunnar Solksjaer.
Kwa mujibu wa Sportsmail imeweka wazi kwamba kocha huyo kwa sasa yupo kwenye mazungumzo na moja ya timu kubwa ambayo itamrejesha kazini hivi karibuni baada ya kukaa bila kazi alipochimbishwa Tottenham, Novemba mwaka jana kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni matokeo mabovu ya timu hiyo licha ya kufanikiwa kuipeleka timu hiyo hatua ya fainali, Ligi ya Mabingwa Ulaya.
0 COMMENTS:
Post a Comment