MABONDIA Ibrahim Class na Dennis Mwale wa Malawi jana wameingia katika vita ya maneno walipokutana uso kwa uso kwa mara ya kwanza kabla ya pambano lao la kesho lililopewa jina la 'The Rumble in Dar'.
Class na Mwale watazichapa kuwania ubingwa wa mabara wa WBF kwenye ukumbi wa Next Door Arena, Dar es Salaam, pambano litakalotanguliwa na mengine nane.
Leo mabondia hao watapima uzito na afya zoezi litakalosimamiwa na Rais wa WBF, Goldberg Howard na kushuhudiwa pia na Scott Farrell ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Global Boxing Stars (GBS).
Wadhamini wa pambano hilo ni hoteli ya Onomo, Benki ya CRDB na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).
Mwale na Class walitambiana jana walipokutana uso kwa uso, Mmalawi akisisitiza kuwa anamheshimu Class ambaye ana rekodi nzuri na ni mzoefu ulingoni, lakini hatarajii rekodi yake ya kutopigwa kuvunjwa na Mtanzania huyo.
“Nitamsambaratisha Class mbele ya mashabiki wake, hilo halina ubishi, nimekuja Tanzania kufanya kazi, nimepambana sana hadi kufikia levo ya kuwa bondia wa kimataifa, ngumi ni maisha yangu naziheshimu,” alitamba Mmalawi huyo.
Class amesema haitotokea apigwe katika ardhi ya nyumbani akisisitiza kwamba Mwale amedandia treni kwa mbele, hivyo kitakachomkuta kesho atakisahau.
Pambano la mabondia hao litashuhudiwa na Kubrat Pulev bondia aliyezichapa na Anthony Joshua hivi karibuni, walipowania mikanda ya ubingwa wa WBA, IBF, WBO na IBO.
Pulev ameambatana na mdogo wake, Tervel atakayezichapa na Vikapita Merero wa Namibia kumsindikiza Class na Mwale alisema pamoja ya kwamba hajui ubora wa mabondia wa Tanzania, lakini hamasa aliyoikuta nchini hapa kwenye masumbwi hakuitarajia.
“Tumekuja kufanya kazi, katika familia yetu hatuna pambano kubwa wala dogo, ndiyo sababu mdogo wangu hajawahi kupigwa, na mimi mbali na Anthony Joshua, hakuna pambano nimewahi kupoteza, hivyo tunakwenda kuendeleza historia hiyo katika ardhi ya Tanzania,” amejinasibu Pulev.
Mpinzani wao amesema pamoja na kwamba anacheza ugenini, lakini yeye ni Muafrika na bila shaka hatowaangusha Waafrika wenzake kutoka Tanzania.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Jackson Group Sports Agency inayoandaa pambano hilo, Kelvin Twissa amesema mabondia kutoka nje ya nchi watakaozichapa kesho wamewasili na leo watapima uzito na afya tayari kupanda ulingoni kwenye pambano hilo ambalo kiingilio kitakuwa Sh 100,000 kwa viti vya kawaida, Sh 150,000, 200,000 na 1.6 Milioni kwa meza.
“Maandalizi yamekamilika na hii itakuwa ni mara ya kwanza katika historia ya Tanzania mabondia wakubwa kutoka nchi tofauti kuja kupigana ugenini.
Mabondia wengine watakaozichapa kesho ni Ardi Ndembo wa DR Congo atakayezichapa na Mtanzania Pascal Enock katika uzito wa juu, Happy Daudi atacheza na bondia wa Zambia Lolita Ndembo katika uzito wa superwelter, Saidi Mrosso atazichapa na Gomatsang Gaasite wa Botswana na Jacob Maganga atazipiga na Hafidhi David.
Nasibu Ramadhani atapigana na Nkosinati Biyana kutoka Afrika Kusini na Stumai Muki atapambana na bondia kutoka Zimbabwe Revai Madondo na Shaban Jongo atacheza na Shawn Miller wa Marekani kuwania ubingwa wa WBF International.
0 COMMENTS:
Post a Comment