January 28, 2021


 
TARATIBU zile ndoto ambazo ulikuwa umeziandika kwenye kile kitabu cha kumbukumbu zinazidi kuyeyuka kwa kuwa muda hausubiri na mapambano lazima yaendelee.

 Ipo hivyo pia kwa wale wachezaji ambao kazi yao ni kusaka ushindi ndani ya uwanja muda wote ili timu yao ipate pointi tatu.

Kuanzia Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Kuu Bara huku kwa sasa vita inayokwenda kuanza ni ya mzunguko wa pili ambao ni muda wa kukamilisha hesabu.

Wapo wachezaji pamoja na benchi la ufundi ambalo kwa mzunguko wa kwanza walikuwa na ndoto za kumaliza wakiwa ndani ya 10 bora ila mipango iligoma wakaishia chini ya nafasi ambazo walikuwa wakizipigia hesabu.

 Ukitazama kwa haraka kwa sasa kuna timu nne chini ambazo zimeanza kupoteza matumaini ya kufanya vizuri kutokana na kasi yao kuwa ya kusuasua.

Itazame Ihefu FC ambayo imekuwa ikipambana kusaka ushindi ila bado ipo nafasi ya 18 inakaribiana na Mbeya City iliyo nafasi ya 17 huku Mwadui ikiwa nafasi ya 16.

Namungo licha ya kuwa na viporo vinne bado imekuwa kwenye kasi ambayo hairidhishi kwani ipo nafasi ya 15 na kibindoni ina pointi zake 18.

Kazi kubwa kwa Kocha Mkuu wa Namungo, Hemed Morroco ni kusaka ushindi kwenye mechi zake zote na asisahau kwamba ana kibarua kwenye mechi za kimataifa.

 Namungo inawakilisha nchi kwenye Kombe la Kimataifa katika Kombe la Shirikisho na inapaswa ifanye vizuri huko pia hivyo sio kazi rahisi kuweza kufikia mafanikio ambayo wanayahitaji ikiwa watashindwa kujipanga.

 Achana na hao kuna zile mbili ambazo ni Gwambina FC ipo nafasi ya 14 na Coastal Union ipo nafasi ya 13, hili eneo pia sio salama yanaweza kuwakuta yale ya Mbao FC ambayo ilishushwa daraja na Ihefu.

 Nafasi ya 13 na 14 ikiwa watasalia hapo mpaka mzunguko wa pili utakapokamilika inamaanisha kwamba wana kazi ya kucheza play off na timu kutoka Ligi Daraja la Kwanza hivyo wakizubaa lolote linaweza kutokea.

 Kikubwa ambacho kipo kwa sasa wachezaji wengi ambao timu zao zipo nje ya 10 bora wanakutana na ushindani mkubwa na makosa yao yanakuwa ni ya kujirudiarudia kushindwa kuwa makini.

Hili limekuwa likisemwa mara kwa mara na Kocha Mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda ambaye alikuwa anasema kwamba wachezaji wake wanarudia makosa jambo ambalo linaigharimu timu yake.

Ninapenda kuzikumbusha timu hizi kwamba ikiwa zitajisahau kwenye mzunguko wa pili kupambana ndani ya uwanja kusaka matokeo chanya kuna suala la kushuka daraja.

Ipo wazi kwamba ni lazima timu nne zishuke daraja na mbili kucheza play off. Kwa zitakazoshuka inapaswa zijipange kwa kuwa huko kuna timu zilishuka bado zinapambana kurejea ndani ya ligi.

 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic