DAKIKA 30 ndizo zitaamua bingwa wa WBF wa Mabara kati bondia Ibrahim Class na Dennis Mwale, leo Ijumaa kwenye Ukumbi wa Next Door Arena, Masaki jijini Dar.Mabondia hao watakata mzizi wa fitina katika pambano la raundi 10 litakalosindikizwa na mengine manane.
Jana mabondia hao walipima uzito na afya tukio lililogubikwa na tambo nyingi, huku Class akiahidi kumaliza pambano mapema.Mabondia hao watazichapa katika pambano la raundi 10 ambalo litapigwa kwa dakika 30, ingawa Class amesisitiza kulimaliza mapema.
Mkurugenzi wa Jackson Group Sports Agency, Kelvin Twissa alisema maandalizi yamekamilika na mabondia wote kutoka nje ya nchi wamewasili tayari kwa pambano hilo lililodhaminiwa na benki ya CRDB, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na Hoteli ya Onomo.
Amesema milango ya Next Door Arena itakuwa wazi saa 10 jioni kwa mashabiki kuanza kuingia na pambano la kwanza litaanza saa moja usiku.Mapambano mengine leo ni kati ya bondia kutoka Bulgaria,
Tervel Pulev ambaye atapambana na Vikapita Merero wa Namibia katika uzito wa Cruiser wakati bondia kutoka DR Congo, Ardi Ndembo atapambana na Mtanzania Pascal Enock katika uzito wa juu.
Bondia wa kike Happy Daudi atacheza na Lolita Ndembo raia wa Zambia katika uzito wa superwelter raundi 8 huku Said Mrosso atazichapa na Gomatsang Gaasite wa Botswana na Jacob Maganga atazipiga na Hafidhi David.
Shaaban Jongo atapigana na Shawn Miller wa Marekani kuwania mkanda wa kimataifa wa WBF wa uzito wa juu, Nasibu Ramadhani atapigana na Nkosinati Biyana kutoka Afrika Kusini, Stumai Muki atapambana na Revai Madondo wa Zimbabwe.
Hiyo ni mara ya kwanza katika historia ya ndondi nchini mabondia kutoka nje ya nchi kuja kuzichapa nchini wote wakicheza ugenini.
Mkuu wa wateja wa Jackson Group Sports, Cynthia Marealle amewaomba mashabiki kufika kwa wingi leo ili kushuhudia mabondia hao wakiwania ubingwa huo.
"Jackson Group Sports imewajali wanawake na ndiyo maana hata kwenye pambano la kwanza, washiriki na kuonyesha uwezo mkubwa. Safari hii tumeongeza idadi ya mapambano kwa lengo la kutoa fursa zaidi,” alisema Cynthia
0 COMMENTS:
Post a Comment