UKURASA wa mwisho wa kitabu cha usajili Bongo ulifunikwa Ijumaa iliyopita saa 5:59 ambao ndiyo ulikuwa muda wa mwisho kwa timu zote kusajili.
Ndani ya wakati huo kuna nyota ambao wameondoka na kwenda
kuanzisha maisha sehemu nyingine. Huko walipoenda kuna kazi ambayo wanatakiwa
kuifanya kwa ajili ya kupata upenyo wa kucheza.
Orodha ya wachezaji hao iko ndefu lakini kwenye makala haya
inakutajia baadhi yao ambao wana changamoto kubwa ya kuifanya kwa ajili ya
kucheza. Twende sawa;
Dickson Job
Ni ingizo jipya ndani ya Yanga inayonolewa na Cedric Kaze
raia wa Burundi. Huyu alikuwa ni tegemeo ndani ya Mtibwa Sugar akiwa amecheza
jumla ya mechi 17 kati ya 18 za Ligi Kuu Bara.
Kwenye makazi yake mapya anakutana na muziki wa mabeki wanne
ambao ni; Bakari Mwamnyeto ambaye pacha yake imejibu na Mghana, Lamine Moro
wengine ni Juma Makapu na Abdalah Shaibu ‘Ninja’.
Kazi yake ya kwanza ni kupambana kuvunja moja ya pacha hizo mbili kisha kugombea kuiingia kikosi cha kwanza huku akipambana na watu ambao wamemzidi umri.
Fiston Abdoul Razak
Straika huyu ndiyo kwanza ameingia ndani ya Yanga na ujio
wake unaifanya Yanga kutimiza jumla ya washambuliaji watano ndani ya kikosi
hicho chenye maskani yake Jangwani.
Anakutana na Ditram Nchimbi, Yacouba Songne, Wazir Junior na
Michael Sarpong ambao wapo wanapambania namba kikosi cha kwanza.
Fiston kazi yake kubwa ni kusawazisha makosa ya wenzake ya
kukosa mabao kwa kufunga lakini kumshawishi kocha Cedric Kaze kumpeleka
moja kwa moja katika 11 ya watakaokuwa wanaanza. Fiston atapambana na Sarpong
mwenye mabao manne ambaye ndiye chaguo la kwanza la Kaze.
Perfect Chikwende
Mwamba huyu raia wa Zimbabwe aliwafanya mashabiki wa Simba
wasilale kwa kuwa alitambulishwa usiku mnene majira ya saa 11:59. Akiwa ametoka
zake FC Platinum anakutana na Miraji Athuman ‘Sheva’ ambaye amerejea kwenye
ubora wake.
Sheva ambaye ni mfungaji bora wa Kombe la Mapinduzi akiwa
ametupia mabao manne amewaka sawa na Francis Kahata ambaye naye amerejea kwenye
ubora.
kushawishi benchi la ufundi kufanya kazi ya ziada kupata
namba kikosi cha kwanza.
Mathias Kigonya
Kipa mfungaji raia wa Uganda alisajiliwa na Azam kwenye siku
za mwishomwisho za usajili na kufanya kikosi hicho kiwe na makipa wanne.
Makipa hao ni Benedict Haule, David Kissu, Wilbol Maseke na
Kigonya. Watatu hao tayari walikuwa wanacheza hivyo Kigonya anahitajika kufanya
kazi ya ziada kwa ajili ya kumshawishi Kocha wake mkuu, George Lwandamina
kumfanya awe chaguo lake lwa kwanza.
Raphael Daud
Hakuwa ndani ya uwanja kwa muda mrefu akimisi mzunguko wote
wa kwanza baada ya kuachwa na Yanga mwanzoni mwa msimu ambapo kwa sasa
ameibukia Ihefu SC ya Mbeya.
Kilichopo mbele yake kwa wakati huu akiwa anasubiri kuvaa
jezi ya klabu yake hiyo mpya ni kumuaminisha Kocha Mkuu, Zuber Katwila kwamba
bado yupo, lakini kuinusuru Ihefu kutoka mkiani mwa ligi.
Peter Manyika
Ndani ya Polisi Tanzania hakuwa na nafasi kutokana na
ushindani wa namba. Amesepa zake na kutua Dodoma Jiji ambapo nako ana kazi ya
kumpiku Aron Karambo ambaye ni chaguo namba moja la Mbwana Makata.
Akishindwa kufanya hivyo basi kile ambacho alikikimbia Polisi
huenda kikajirudia kwa kuwa na urafiki na benchi.
Stamili Mbonde
Hakuwa na timu baada ya kuachwa na Mtibwa Sugar mwishoni mwa
msimu uliopita, sasa anaibuka ndani ya Tanzania Prisons inayotumia Uwanja wa
Nelson Mandela.
Anakwenda kusaka nafasi mbele Jeremiah Juma ambaye ni
mshambuliaji chaguo namba moja la kocha Salum Mayanga.
Yahya Zayd
Kiungo huyu mshambuliaji kazi yake kubwa ni kusaka nafasi ya
kucheza ili mabosi wake waliomchukua kwa mkopo Azam FC wasione kwamba ni mzigo
na mabosi wake wa Misri, Pharco washtuke kwamba mwamba huyu anayaweza uwanjani.
Erick Kwizera
Wanamuita Messi wa Burundi ambaye aliuwasha kwelikweli kule
Mapinduzi Cup na kuwafanya mabosi wa timu hiyo kumpa mkataba. Sasa baada ya kula
maisha ana kazi ya kufanya ya kupambana kucheza kikosini lakini kuifanya timu
hiyo iwe tishio Afrika.
Ataanza kutumika katika hatua ya 32 bora ya Kombe la
Shirikisho Afrika ambapo Namungo wamepangwa kucheza na C.D. Primeiro de Agosto
ya Angola na kwenye ligi.
0 COMMENTS:
Post a Comment