JOTO limezidi kutanda kuelekea mechi ya kirafiki kati ya Global FC dhidi ya timu ya DSTV mchezo unaotarajiwa kupigwa kesho kutwa Jumapili kwenye Viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, manahodha wa timu zote mbili wamezidi kupigana mikwara kuelekea mchezo huo.
Mchezo huo ambao ni maalum kwa ajili ya kudumisha uhusiano na ujamaa kati ya Kampuni ya Multichoice na Global Group ambazo zimekuwa zikishirikiana kwenye mambo mbalimbali unatarajiwa kuwa na upinzani wa aina yake kutokana na maandalizi ya timu zote mbili.
Akizungumza na Championi Ijumaa kwenye kipindi cha Katambuga kinachoruka hewani kupitia +255 Global Radio nahodha msaidizi wa timu ya Global FC, Marco Mzumbe alisema:
“Kwanza kabisa tunawapa tahadhari DSTV waje kwa nidhamu kwenye mchezo huo kutokana na maandalizi ambayo tumeyafanya wakipona sana tunawafunga mabao saba, kikosi chetu kipo kambini tangu wiki iliyopita kinaendelea na maandalizi chini ya kocha mkuu Philip Nkini.
“Hadi sasa hakuna majeruhi yeyote kwa mujibu wa ripoti ya daktari wa timu, hivyo niwaambie tu DSTV shughuli za wanaume hawapewi wavulana, tumejipanga kuibuka na ushindi mnono siku hiyo.
”Aidha, kwa upande wa nahodha wa DSTV, Festo Laizer alisema: “Tumezisikia tambo zenu tangu wiki iliyopita, lakini tunawakumbusha kuwa mpira hauchezwi mdomoni, kama mlivyojiandaa na sisi tumejiandaa vilevile kikubwa tukutane uwanjani ili tujue nani aliyefanya maandalizi bora.
“Niwaombe mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi siku hiyo kwani mbali na mechi kutakuwa na burudani nyingi nje ya uwanja hivyo hii si ya kukosa.”Kikosi cha Global FC kitaendelea na mazoezi ya mwisho leo Ijumaa kuelekea mchezo huo utakaoanza saa 3:30 asubuhi.
0 COMMENTS:
Post a Comment