MCHAKATO wa kuboresha vikosi kupitia dirisha dogo la usajili umekamilika rasmi jana baada ya kudumu kwa kipindi cha takribani mwezi mmoja tangu lilipofunguliwa Desemba 16.
Ligi ya msimu huu imeshuhudia kuwepo kwa ushindani mkubwa
kutoka kwenye timu shiriki ambazo zinaonekana kushindana na sio kushiriki.
Mara nyingi imezoeleka kuona mastaa wa klabu za Simba, Yanga
na Azam wakifanya vizuri kuzidi mastaa wa vikosi vingine, lakini wapo baadhi ya
nyota kutoka nje ya vikosi hivyo ambao wamekimbiza kwelikweli ndani ya mzunguko
wa kwanza msimu huu.
Hii hapa listi ya baadhi ya nyota ambao hawaundi vikosi vya
Simba, Yanga na Azam lakini walikiwasha kwelikweli na wanatarajiwa kufanya
makubwa msimu huu kama ifuatavyo;
Adam Adam (JKT Tanzania)
Anakamatia nafasi ya pili kwenye msimamo wa chati ya
wafungaji bora msimu huu ambapo mpaka sasa amefanikiwa kuweka kambani mabao
saba, tofauti ya bao moja tu na kinara wa msimamo na nahodha wa Simba, John
Bocco mwenye mabao nane.
Ukiachana na mabao hayo saba aliyofunga, Straika huyo wa JKT
Tanzania ametoa pasi moja ya bao hivyo kumfanya ahusike kwenye jumla ya mabao
nane kwenye ligi msimu huu.
Uwezo mkubwa aliouonyesha Adam umemfanya kocha wa timu ya
Taifa, Etienne Ndayiragije amjumuishe kwenye kikosi cha Stars ambacho kilicheza
michezo ya kufuzu AFCON dhidi ya Tunisia mwezi Novemba.
Steven Sey (Namungo)
Straika Mghana wa klabu ya Namungo ambaye amejipatia umaarufu
mkubwa kutokana na staili yake ya kuchomekea, na kupungia mkono wapinzani kila
anapowafunga bao.
Sey aliyesajiliwa msimu huu kutokea Singida United amekuwa na
mwanzo mzuri wa msimu ambapo mpaka sasa ameifungia Namungo mabao tisa.
Mabao matatu amefunga kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara, huku
mabao manne akifunga kwenye mchezo wa awali wa michuano ya kombe la Shirikisho
Afrika huku mabao mawili akifunga kwenye michuano ya kombe la Mapinduzi.
Kutokana na uwezo wake mkubwa tayari klabu kadhaa zimeonyesha
nia ya kumuhitaji kwa ajili ya kuboresha vikosi vyao, miongoni mwa klabu
zinazotajwa kuhitaji huduma yake ni vinara wa msimamo Yanga.
David Luhende (Kagera Sugar)
Beki huyu wa kushoto wa Kagera Sugar anatajwa kuwa kwenye
mipango ya kusajiliwa kwa mara nyingine tena na vinara wa msimamo wa ligi klabu
ya Yanga, ambayo aliwahi kuitumikia miaka ya 2013.
Hii ni baada ya nyota huyo kuonyesha kiwango kikubwa msimu
huu akihusika kwenye mabao matano ya Kagera Sugar, amefunga bao moja na kuasisti
mabao manne.
Unaweza kusema ameanzia alipoishia, kwani msimu uliopita
aliweka rekodi ya kucheza michezo yote 38 ya Kagera Sugar kwa kiwango kikubwa,
kiasi cha kuingia kwenye kinyang’anyiro cha mabeki bora watatu wa msimu.
Yusuph Mhilu (Kagera Sugar)
Msimu uliopita alimaliza akiwa katika nafasi ya tatu kwenye
chati ya wafungaji bora baada ya kuweka kambani mabao 13.
Msimu huu haujaanza vizuri kwa upande wake kwani amekuwa
akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara yaliyomfanya akose baadhi ya michezo
ya Kagera Sugar.
Licha ya kukosa sehemu kubwa ya michezo muhimu ya Kagera
Sugar ikiwemo mchezo dhidi ya Ihefu, lakini nyota huyo hajatetereka ambapo
mpaka sasa amefanikiwa kuweka kambani mabao manne.
Meshack Abraham (Gwambina)
Tayari jina lake linaonekana kuwavutia wababe wa Kariakoo,
ambao wameonyesha nia ya kuhitaji huduma yake kwa ajili ya kuboresha vikosi
vyao kuelekea mzunguko wa pili wa ligi.
Hii ni baada ya nyota huyu wa Gwambina kuweka kambani mabao
sita mpaka sasa, akiwa kwenye nafasi ya nne kwenye chati ya wafungaji msimu
huu.
Abraham yupo sawa na kinara wa ufungaji ndani ya Azam, Prince
Dube ambaye naye ameweka kambani mabao sita wote kwa pamoja wakizidiwa mabao
mawili tu na kinara wa wafungaji Bocco.
Fully Maganga (Ruvu Shooting)
Dakjika ya 35 ni dakika mbaya zaidi kwa Simba pale inapocheza
dhidi ya Ruvu Shooting, lakini ni dakika nzuri zaidi kwa nahodha wa maafande
hao, Fully Maganga ambaye ndani ya michezo miwili mfululizo iliyopita dhidi ya
Simba amefanikiwa kuifunga mabao mawili.
Juni 14, msimu uliopita aliifungia Ruvu bao la kusawazisha
dhidi ya Simba, huku Oktoba 26 msimu huu akirejea tena kufanya hivyo mchezo
ulioisha kwa Simba kufa bao 1-0.
Maganga mpaka sasa amefanikiwa kuweka kambani mabao matano na
kukamatia nafasi ya kumi kwenye chati ya wafungaji bora msimu huu.
0 COMMENTS:
Post a Comment