USHINDANI ndani ya uwanja kwa msimu huu wa 2020/21 unaonekana wazi kwamba ni mkubwa na hili ni jambo jema kwa afya ya soka letu la Tanzania.
Ikumbukwe
kwamba msimu wa 2019/20 ambao ulikamilika licha ya changamoto mbalimbali ambazo
zilijitokeza ulikuwa na ushindani mkubwa.
Kila timu
ilikuwa inapambana ndani ya uwanja kusaka ushindi na mwisho wa siku matokeo
yataamua nani awe bingwa. Pia wapo ambao watamaliza safari yao ndani ya ligi na
kuibukia Ligi Daraja la Kwanza.
Kuna kazi
kubwa ambayo inapaswa ifanyike pia kwa timu ambazo zimekuwa hazipati matokeo
chanya ndani ya uwanja. Hakuna timu ambayo inakubali kupoteza kirahisi hivyo
hapo lazima ushindani uwe mkubwa.
Kwa
kuonyesha ushindani ndani ya uwanja kutafanya maisha ya soka la Tanzania kuzidi
kupasua anga kitaifa na kimataifa kwa kuwa kila timu itakuwa inapambana ndani
ya uwanja kusaka matokeo.
Kwa timu
ambazo matokeo yao yamekuwa ni ya kusuasua ni muhimu kuongeza nguvu kwenye
mzunguko wa pili ili kuweza kupata matokeo chanya.
Inawezekana
kwa kila timu kuweza kuwa kwenye mabadiliko ndani ya uwanja na kupata matokeo
ambayo ni mazuri pale ambapo wataamua na mwisho wa siku watarejesha tabasamu
kwa mashabiki wao.
Mashabiki
wanapenda kuona ligi yenye ushindani inayovutia kuitazama kila siku na sio kila
baada ya mechi kuisha mtu unajutia kwa nini ulipoteza muda wako.
Maboresho
yaanze kuanzia ndani ya uwanja na kabla ya mechi, kila mechi ipewe kipaumbele
sawa bila kubagua aina ya timu kama tabia hii itaendelea itapoteza ule
ushindani.
Pia tunaona
kwamba kuna Kombe la Shirikisho ambalo linaendelea pia kwa timu kupambania
nafasi zao za kuweza kutwaa taji hilo kubwa na lenye heshima.
Katika hili
ni muhimu kila mmoja akaweza kujipanga vema kwenye mashindano haya na kuwekeza
nguvu pia huku kwani wapo ambao wamekuwa wakipuuzia.
Ukitazama
namna wawakilishi wa Tanzania Namungo wanafanya vizuri kimataifa njia yao ya
kufika huko ilikuwa ni kwenye Kombe la Shirikisho ambalo wapo ambao wanaliona
ni la kawaida.
Muhimu kwa
timu shiriki ni kuwekeza nguvu pia huku ili waweze kupata matokeo mazuri ndani
ya uwanja. Ili kupata matokeo mazuri ni lazima kuwe na maandalizi mazuri.
Ikiwa timu
itapata muda wa kufanya maandalizi mazuri itakuwa na nafasi ya kupata matokeo
chanya ndani ya uwanja.
Kila kitu
ndani ya uwanja kinahitaji utulivu pamoja na umakini. Kupata matokeo mazuri ni
jambo ambalo linahitaji maandalizi hivyo ni muhimu kwa kila timu kuanza
kutazama jambo hili kwa ukaribu.
Mashabiki
nao wana kazi ya kuendelea kuzipa sapoti timu zao ndani ya uwanja ili kuweza
kuongeza hamasa kwani mpira unahitaji mashabiki pamoja na zile shangwe za
mashabiki.
Bado imekuwa
ikionekana kwamba mchezo wa fainali unapelekwa mbali na Dar ikiwa ni sera ya
kukuza soka na kupekeka burudani kule ambako bado hakujawa na shangwe la
kutosha.
Katika hili
bado tunahitaji kujifunza zaidi ili kuwa bora kwa kuwa haya mashindano ya FA
siyo madogo na kila mmoja ana kazi ya kujua namna gani hili linaweza kuwa bora
zaidi kwa wakati ujao.
Tujifunze
kwa wenzetu Uingereza lazima fainali ya FA ichezwe Wembley, maana yake nini
mchezaji anakuwa anaona fahari kucheza kwenye uwanja mkubwa wenye hadhi sawa na
mashindano yenyewe.
Sasa leo
sisi tunapeleka fainali Lindi, Kigoma, Rukwa hata Mbeya pia inaweza kufika ila
hapo jambo la kujiuliza ni kwamba sehemu ya kuchezea ina hadhi ya kimataifa?
Bado fainali
itabaki kuwa fainali kwa kuwa kuna mengi ambayo yanafanyika kisha namna
wachezaji ambapo wanapambana kufika hapo na mwisho wa siku wanacheza kwa
kujilinda zaidi wasitoe burudani kutokana na tatizo la uwanja.
Kila kitu ni
mipango hivyo kwa sasa ni muhimu maboresho yakafanyika na kukawa na utaratibu
mzuri kwa ajili ya kuwa na sehemu nzuri ya kuchezea fainali ya FA.
Fainali huwa
inafuatiliwa na wengi hivyo ikiwa itachezwa sehemu nzuri ya uwanja itatoa fursa
kwa wachezaji kuwa sokoni na kucheza kwa kujiamini mwanzo mwisho.
Ifike wakati
iwe inajulikana kwamba kama ni fainali ya FA lazima ifanyike kwenye uwanja wa
Taifa kwa kuwa una hadhi ya kimataifa itatoa heshima kwa timu ambazo
zinashiriki michuano hiyo.
Muda ni sasa
wa TFF kufanyia maboresho haya matatizo ambayo yanajitokeza mara kwa mara na
kusimamia vitu vya soka kwa utaratibu ambao unaleta matokeo bora.
Kila kitu
kinawezekana endapo tutaamua mwisho wa siku suala la ratiba nalo linapaswa
litazamwe kabla ya kupanga mechi ambazo ni muhimu kwa kila timu kupata ushindi.
0 COMMENTS:
Post a Comment