DIDIER Gomes, Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa wachezaji wake wote ikiwa ni pamoja na Luis Miquissone ambaye ni kiungo pamoja na Chris Mugalu ambaye ni mshambuliaji huwa wanafanya mazoezi maalumu ya kupiga penalti.
Mugalu alikosa penalti kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara mbele ya Tanzania Prisons ambapo ilikwama kwenye mikono ya kipa wa Prisons, Jeremiah Kisubi.
Kwa sasa Simba ina kibarua cha kusaka ushindi mbele ya AS Vita ambao ni mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika unaotarajiwa kuchezwa Aprili 3, Uwanja wa Mkapa.
Gomes raia wa Ufaransa ameliambia Spoti Xtra kuwa anawaandaa wachezaji wake wote wawe imara kwa ajili ya matumizi ya mipira ya kutengwa ili waweze kupata matokeo chanya.
“Nimekuwa nikiwaambia kwamba jukumu la kupiga mipira ya kutengwa ni ya kila mchezaji, awe ni Luis, Mugalu ama Chama (Clatous) ni jukumu la timu na ni jambo ambalo tumekuwa tukifanyia mazoezi.
“Lengo la kuwapa mazoezi hayo ni kuona kwamba tunaweza kufunga kwa namna yoyote ile iwe ni kwa kutengeneza njia za kufunga ama kufunga kwa mipira ya kutengwa,” alisema.
Pia hata Chama naye alikosa penalti kwenye mchezo wa ligi mbele ya Azam FC kwenye sare ya kufungana mabao 2-2, Uwanja wa Mkapa.
0 COMMENTS:
Post a Comment