Na Saleh Ally
MWAKA 2017, ndiyo Klabu ya
Simba iliingia mkataba wa miaka mitano na kampuni kubwa ya masuala ya michezo ya
kubahatisha ya SportPesa Tanzania.
Mkataba wa udhamini ambao
unaifanya Simba na watani wao Yanga kuingia kwenye rekodi mpya ya klabu zenye udhamini
mkubwa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwa zinapokea kitita cha
hadi Sh bilioni 1.3 kwa mwaka mmoja, haijawahi kutokea katika soka nchini.
SportPesa imeandika rekodi ya
kuwa kampuni inayotoa udhamini mkubwa zaidi nchini katika michezo na Simba ni
timu ambayo imeutumia vizuri zaidi udhamini huo kujikomboa kuliko watani wao wa
jadi, Yanga.
Simba sasa ni tishio, si
Tanzania pekee, bali Afrika Mashariki na Kati na gumzo Afrika lakini hakuna
ubishi kwamba wadhamini wao wakubwa na waliosaidia mabadiliko makubwa wakiwa
chachu ni SportPesa.
Wakati Sportpesa wanaingia mkataba wa kuidhamini Simba mwaka 2017, Simba ilikuwa haijagusa ubingwa wa Tanzania Bara kwa misimu minne mfululizo. Katika misimu hiyo minne, watani wao wa jadi Yanga walikuwa wameubeba ubingwa huo kwa mara tatu mfululizo na Azam FC mara moja.
Achana na hivyo, kuna wakati hata
kushika nafasi ya tatu ilikuwa shida. Kama unakumbuka msimu wa 2013/14, mabingwa
walikuwa ni Azam FC, wakafuatiwa na Yanga halafu Mbeya City na Simba wakitupwa
nje ya tatu bora ya Ligi Kuu Bara.
Msimu uliofuata wa 2014/15, Simba
ikarejea katika kiwango cha nafuu na kufanikiwa kushika nafasi ya tatu huku
Yanga wakiwavua ubingwa Azam FC ambao walirudi katika nafasi ya pili.
Safari ya mapambano ikahamia
2015/16, Yanga wakaendeleza ubabe, Azam FC wakabaki nafasi ya pili na Simba
wakaendelea kubaki katika nafasi ya tatu.
Msimu wa 2016/17, Simba
wakajitutumua na kupanda hadi katika nafasi ya pili huku Kagera Sugar
wakiiondoa Azam FC katika nafasi ya tatu. Hata hivyo, Simba haikuweza kuivua
Yanga ubingwa baada ya kulingana pointi lakini mabao ya kufunga na kufunga
yakawa ni mzozo.
Huu ndiyo msimu wa nne wa Simba
kabla ya SportPesa kuingia nao mkataba mwaka 2017, wakati ambao safari ya
mabadiliko ya maisha mapya ya kikosi hicho yalianza.
Rafiki yangu mmoja mdau wa
mpira aliwahi kuniambia anachukizwa na viongozi wa Simba wanavyoichukulia poa
SportPesa. Kwamba hawaijali au kuitimizia mambo kadhaa, sikuwa na uhakika kama
hilo linatokea. Lakini nikamuambia kama wanafanya hivyo, basi watakuwa wasahaulifu
au wanajisahaulisha.
Sijawahi kuwasikia SportPesa
wakilalamika kuhusiana na Simba kutotimiza yaliyo katika mkataba lakini kama ni
hivyo, hata wao wanatakiwa kukumbuka kwa kuwa safari waliyosafiri na SportPesa
imekuwa na mafanikio makubwa.
Umeona misimu minne waliyokosa
ubingwa na mara moja hata katika tatu bora wakiwa nje. Lakini misimu minne ya
SportPesa, mfululizo mara tatu wamechukua ubingwa na dalili zote kuwa msimu
wanne ambao ni huu, wanaweza kuwa mabingwa tena.
Safari ilianza 2017/18 na Simba
wakabeba ubingwa wakiwa na pointi 69 mwishoni mwa msimu, nafasi ya pili ikaenda
Azam FC wakiwa na pointi 58 na watani wao Yanga wao baada ya kubeba ubingwa
mara tatu mfululizo, wakavuliwa na kutulia katika nafasi ya tatu wakiwa na
pointi 52.
Msimu uliofuata ukiwa wa pili
wakiwa na Sportpesa, yaani 2018/19, Simba wakabeba tena ubingwa, msimu huu
wakiwa moto zaidi baada ya kukusanya pointi 93, Yanga wakapanda hadi nafasi ya
pili wakiwa na 86 na Azam FC wakashuka hadi namba tatu wakiwa na pointi 75.
Simba hawakupunguza kasi, msimu
wa 2019/20, wakachukua ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo na kuwajibu watani
wao Yanga. Safari hii wakiwa na pointi 88, Yanga wakafuatia wakiwa na 72 na
Azam FC pointi 70, wakiwa katika nafasi ya tatu.
Sasa ni msimu huu wakiwa
wanaonekana pia wana nafasi ya kuwa mabingwa tena na wapinzani wao wakiwa watani
wao Yanga. Katika misimu hii minne, Simba wameandika rekodi ya kipekee.
Wamecheza Ligi ya Mabingwa na kufanikiwa kufika hatua ya robo fainali mara
mbili, kumbuka mara ya mwisho kuingia hatua ya robo fainali ilikuwa ni mwaka 2003.
Bila ya ubishi, Simba bora
zaidi ni hii ambayo imepatikana katika kipindi wadhamini wakuu wakiwa ni
SportPesa, hakuna ambaye anaweza kuwatoa katika historia ya hili lililotokea.
Simba ya msimu wa 2020/21, ndiyo
bora zaidi kwa maana ya kiwango. Kwa wale ambao walikuwa wakipinga, hakuna
anayesema tena, hakuna anayeinua mdomo na kusema inapendelewa, hakuna
anayejaribu kusema inabahatisha badala yake kila mmoja asiyependa mwendo wa
Simba anachofanya labda iwe dua mbaya kimyakimya.
SportPesa wapo katika historia
na rekodi hii, inawezekana wako wanaotaka kupinga lakini viongozi na mashabiki
wa Simba wanalijua hilo Viongozi wa Simba wanastahili pongezi kubwa, maana unaweza
kusema vipi Yanga, kwani nao wanapewa udhamini kama huo wa SportPesa lakini
vipi. Kweli, viongozi wa Simba wamekuwa bora zaidi na walichofanya pamoja na
ubora wa mambo mengine, wameutumia vizuri sana udhamini wa SportPesa pamoja na
nyongeza kutoka Azam TV na Mo Xtra kuunganisha nguvu na kufanya mambo yaende
kwa uhakika zaidi.
Si vibaya kusema Simba hii ya
kipindi cha SportPesa, imekuwa Simba hasa na yenye mafanikio makubwa na tayari
historia ya Simba na kampuni hiyo kubwa ya michezo ya kubahatisha hakuna
anayeweza kuifuta.
SportPesa imebadilisha mambo
kadhaa katika mpira wa Tanzania kama ambavyo unaona iliweza kuzidhamini timu
kadhaa na Namungo FC imekuwa moja ya timu
zilizoandika rekodi ya kuingia
hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
Hatua hiyo si ndogo, ni kubwa
tena sana na hasa kwa timu kama Namungo FC ambayo hata katika Ligi Kuu Bara ni
wageni. Unaona, ndani yake kuna mchango wa
SportPesa kama sehemu ya
wadhamini na hii inakufanya uone kweli, mchango wa kampuni hiyo ni mkubwa sana
na umesaidia kuleta mabadiliko
makubwa katika mpira wa Tanzania. Achana na kwamba walizidhamini timu kama
Singida United na zikawa tishio, lakini historia ya kampuni hiyo na udhamini
wake Simba, itaendelea kuzungumza kwa
miaka mingi sana ijayo na jezi
yenye SportPesa kifuani, itapita katika miaka mingi ya historia ya Simba na
soka la Tanzania, kama kumbukumbu yenye mifano isiyoisha.
0 COMMENTS:
Post a Comment