MASTAA wa kimataifa wa Yanga akiwemo Fiston Abdoul Razack na Michael Sarpong, huenda wakakutana na makato ya mishahara yao ya kila mwezi kama timu hiyo ikiendelea na matokeo yasiyoridhisha.
Hiyo ikiwa ni siku chache tangu Yanga itoke kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya KMC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Mara baada ya mchezo huo, mashabiki wa Yanga walionekana kulalamikia viwango vibovu ambavyo wachezaji wao wamevionesha.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, uongozi wa timu hiyo umepanga kufuata makubaliano yaliyopo kwenye mikataba waliyoingia nayo wachezaji hao.
Mtoa taarifa huyo alisema katika mikataba hiyo waliyoingia nayo wachezaji hao wa kimataifa ni pale wanaposhindwa kuisaidia timu na kuonyesha kiwango, basi watakatwa mishahara kwa kiasi walichokubaliana.
Aliongeza kuwa, wachezaji ambao huenda wakakutana na makato hayo ni Fiston na Sarpong wanaocheza nafasi ya ushambuliaji.
“Kwa jinsi inavyoelekea uongozi utarejea kwenye makubaliano ya awali yaliyowekwa katika mikataba ya wachezaji wao wote waliosajiliwa msimu huu.
“Makubaliano yaliyowekwa awali katika mikataba yao ni kama mchezaji atashindwa kuisadia timu au kiwango chake kushuka kwa washambuliaji kushindwa kufunga mabao, basi watatakiwa kukatwa mishahara.
“Hayo makubaliano yalikuwepo tangu awali, lakini viongozi waliwaachia licha ya wachezaji hao kushindwa kutimiza majukumu yao na hiyo imetokana na baadhi ya wachezaji viwango vyao kushuka,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla kuzungumzia hilo, hakupatikana na hakuna kiongozi mwingine wa Yanga aliyekuwa tayari kuzungumza.
0 COMMENTS:
Post a Comment