May 18, 2021


 MEI 15 katika Uwanja wa CCM Gairo jijini Morogoro, Klabu ya Geita Gold ilifanikiwa kutegua kitendawili cha muda mrefu, juu ya nani anaungana na kikosi cha Mbeya Kwanza kupanda daraja na kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Geita Gold imepanda daraja baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fountain Gate, katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Gairo mkoani Morogoro.

Matokeo hayo yamewafanya Geita kufikisha pointi 37 ambazo haikuwezekana kufikiwa na klabu nyingine yoyote, ikiwemo waliokuwa washindani wao wa karibu klabu ya soka ya Pamba ambao wamemaliza wakiwa na pointi 36.

Bila shaka Klabu ya Geita Gold na Mbeya Kwanza wanastahili pongezi nyingi kwa kufanikisha lengo lao kubwa msimu huu.

Kwa namna ushindani wa Ligi Daraja la Kwanza unavyojulikana na watu wengi, hapana shaka sote tunakubaliana kuwa klabu hizi zimeruka vigingi vingi mpaka kufika walipo sasa.

Baada ya kupokea pongezi hizo, naamini sasa ni muda muafaka kwa klabu hizo kuanza maandalizi ya Ligi Kuu ya msimu ujao. Shangwe lisiwe jingi bali kazi ya kutengeneza njia yao kuelekea michezo ya Ligi Kuu ndilo jambo la muhimu.

Wageni hawa wa ligi wanapaswa kuelewa kuwa wanakotoka na wanakoelekea ni mahali tofauti sana, yaani ushindani wa Ligi Daraja la Kwanza ni tofauti sana na ule wa Ligi Kuu.



Hivyo litakuwa jambo la hekima kwao kama wataacha kufanya mambo kwa mazoea, na kujipanga upya kwa ajili ya hatua kubwa waliyoiingia.

Kama watachukulia mambo kwa mazoea na kudhani kuwa nguvu waliyoitumia katika Ligi Daraja la Kwanza kuelekea Ligi Kuu pekee inatosha, basi pasi na shaka watabaki wamepigwa butwaa mwisho wa msimu.

Ipo nadharia kuwa kupanda Ligi Kuu kutokea madaraja ya chini ni jambo rahisi zaidi, kuliko kushuka kutoka Ligi Kuu na kupanda tena, hivyo hili ni somo ambalo Geita Gold na Mbeya Kwanza wanapaswa kuwa nalo kabla ya kuanza kwa Ligi.

Bila shaka hili linathibitishwa na Klabu za Alliance na Mbao ambazo kwa bahati mbaya sana kwao, wamezidi kushuka chini wakienda Ligi Daraja la Pili (SDL), ikiwa ni msimu mmoja tu umepita tangu wawe washiriki wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita wa 2019/20.


Hivyo chaguo ni lao iwe kusuka au kunyoa, kwani kujifunza ni jambo la hiyari zaidi kuliko lazima. Binafsi naendelea kuzipongeza timu zote mbili, kuwakumbusha wajibu wao na kuzitakia kila la kheri kuelekea ukurasa wao mpya wa kucheza Ligi Kuu Bara, naitazamia Ligi Kuu Bora kwa msimu ujao wa 2021/22 panapo majaaliwa ya uhai.


 


 


 


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic