NGUVU kubwa kwa sasa kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara ni kuona namna gani zinaweza kupata kile ambacho wanastahili mara baada ya msimu wa 2020/21 kukamilika.
Mbali na Mwadui FC ambayo hesabu zimeigomea kubaki ndani ya ligi licha ya mechi zake nne mkononi bado kuna timu nyingine ambazo zitashuka pia.
Ligi Daraja la Kwanza zitapanda mbili jumla huku nne zikishuka ambazo ni timu kutoka Ligi Kuu Bara na msimu ujao zitashiriki ligi hiyo ambayo nayo ushindani wake sio wa kawaida.
Shirikisho la Soka Tanzania,(TFF) liliweka wazi tangu awali mpango wa kupunguza timu kutoka 18 mpaka 16 ambapo zile zitakazokuwa nafasi ya 13 na 14 zitacheza playoff.
Kwa zile ambazo zitashuka zina jukumu la kujipanga upya na kufanya kazi kwa umakini katika kutimiza majukumu yao kwa sababu huku juu ushindani ni mkubwa muda wote.
Nimekuwa nikiwasiliana na marafiki zangu wengi kutoka nje ya nchi ambao wanatupa pongezi nyingi kwa kuwa na maendeleo kwenye suala la mpira kwa kuwa wanaona kupitia Azam TV.
Hili ni jambo la kujifunza pia kwa wachezaji wetu kuzidi kuonyesha ule uwezo wao wa asili pale wanapopewa nafasi ya kuanza ndani ya timu jambo litakalowaweka sokoni kwa wakati ujao.
Mbali na ligi pia kuna mashindano ya Kombe la Shirikisho ambalo nalo pia kila timu inalitazama taji hilo ili kuweza kuwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa.
Namungo waliweza kupeperusha bendera ya Tanzania katika Kombe la Shirikisho baada ya kuwa ni washindi wa pili na Simba ilisepa na taji hilo ila tayari kwenye hatua ya 16 bora imeondolewa.
Hapo kuna jambo ambalo lipo kwa Namungo kwa msimu huu kwa kuwa wametinga hatua ya makundi Kombe la Shirikisho ila walikwama kukusanya pointi.
Kwa kutinga hatua ya makundi wanastahili pongezi ila kukwama kukusanya pointi wanapaswa kujiuliza mara mbilimbili ilikuaje wakashindwa kujitutumua katika hatua hiyo kubwa.
Kwa namna ushindani ulivyo msimu huu ikiwa Namungo pamoja na timu nyingine zitashindwa kuongeza juhudi basi mwisho tutakusanya maumivu kwa timu mbalimbali ndani ya ardhi ya Bongo.
Kwa wakati huu timu ambazo zipo kwenye lala salama basi zina kazi ya kuanza kujipanga upya angalau kupata kitu katika mechi hizi kwani maumivu hayaepukiki kwa namna yoyote ile.
Uzuri ni kwamba kabla ya msimu huu kuanza tuliongea kuhusu mipango ili kuona kwamba namna gani timu inaweza kupata matokeo chanya.
Kwa kilichotokea mwanzo kwa wakati huu hakuna namna ya kubadili zaidi ya kuona kwamba kila mmoja anavuna kile ambacho anakipata.
Suala la kushuka haliepukiki kwa namna yoyote ile jambo la msingi ni kujipanga vema ili kuweza kuwa imara.
Inawekezana zipo timu ambazo zipo mahali hapo kwa sasa kutokana na kushindwa kupata matokeo mazuri awali hivyo kama wakipata nafasi msimu ujao watakuwa na kazi ya kujipanga.
Kazi kubwa itakuwa kurekebisha yale makosa ambayo waliyafanya wakashindwa kufikia malengo ambayo walikuwa wamejipangia.
Wachezaji ambao walishindwa kuonyesha uwezo wao ni muda wao wa kupata changamoto mpya katika sehemu ambayo inawastahili tofauti na maisha ambayo waliishi wakati uliopita.
Kwenye maisha ya soka kila kitu kinawezekana na mambo kubadilika ni mara moja tu hivyo ikiwa walipata nafasi wakashindwa kuzitumia bado wana nafasi nyingine ya kuonyesha huko ambako watakwenda.
Wapo ambao watakwenda kwenye baadhi ya timu kwa mkopo na wapo ambao watakwenda katika timu zingine kupata changamoto mpya.
Jambo la msingi msimu ujao wakipata nafasi basi wasichezee fursa hiyo kazi yao iwe moja tu kupambana kwa hali na mali kusaka ushindi kwa ajili ya timu zao.
Furaha ya mashabiki imejificha kwenye matokeo chanya na furaha ya wachezaji wao ipo kwenye kucheza na kupata matokeo mazuri, hakuna jambo jingine.
0 COMMENTS:
Post a Comment