ZILE shangwe za mashabiki ambazo zilikuwa zinazunguka kwenye vichwa vya wachezaji na purukushani za mashabiki kupata burudani sasa zimerejea.
Vita kubwa inaendelea pale ambapo iliishia msimu uliopita wa 2020/21 uliokuwa na ushindani mkubwa hivyo ni suala la kusubiri nani atakuwa nani baada ya msimu kukamilika.
Hapa Spoti Xtra inakuletea namna vita itakavyoanza upya kwa msimu ndani ya ligi ambayo ilianza kutimua vumbi Septemba 27 baada ya mchezo wa ufunguzi wa ligi ule wa Ngao ya Jamii kuchezwa na ubao wa Uwanja wa Mkapa kusoma Simba 0-1 Yanga:-
Kiatu cha ufungaji bora
Mbio hizi kwa msimu wa 2020/21 zilipamba moto na mwisho wa siku ziliangukia kwenye miguu ya nyota wa Simba, John Bocco ambaye alifunga jumla ya mabao 16.
Licha ya kwamba alikuwa ni namba moja bado waliomfuatia ndani ya tatu bora walikuwa sio haba, alikuwa ni Chris Mugalu huyu alitupia mabao 15 yupo Simba na namba tatu ilikuwa kwenye miguu ya Prince Dube yupo zake Azam FC.
Nyota wa Simba kwa sasa wote wapo fiti ila Dube atakuwa nje kwa muda akitibu majeraha yake hivy atakosekana kwenye mechi za mwanzo.
Mkali wa kutengeneza pasi za mwisho
Mwamba wa Lusaka ambaye alikuwa akiwakimbiza wazawa, Clatous Chama kwa sasa hayupo ndani ya Simba hivyo mfalme mpya anatafutwa kukabidhiwa mikoba.
Kwa msimu uliomeguka kabla ya Chama kuibukia ndani ya RS Berkane alitupia jumla ya pasi 15 na alitupia mabao 8 na alikuwa ni namba moja kwa watengeneza pasi za mwisho na mshikaji aliyemfuatia alikuwa ni Luis Miquissone huyu yeye alitoa jumla ya pasi 10 na alifunga mabao 9 naye yupo zake Al Ahly ya Misri.
Vita hapa ni kwenye msako wa mkali mpya wa pasi za mwisho.
Kipa bora
Aishi Manula amekuwa akifanya vizuri muda wote ndani ya Ligi Kuu Bara akiwa na tuzo ya kipa bora kwa msimu uliopita baada ya kukusanya jumla ya clean sheet 18.
Uwepo wa Metacha Mnata ndani ya Polisi Tanzania,Faroukh Shikalo ndani ya KMC, Diarra Djigui ndani ya Yanga ni viashiria kwamba vita ya kipa bora itakuwa kwenye ushindani mkubwa.
Beki bora
Hapa ile safu ya Simba inayoongozwa na Joash Onyango pamoja na Pascal Wawa ilikuwa ni namba moja kwa kuwa iliruhusu mabao 14 kwenye mechi 34 ilifuatiwa na Yanga inayoongozwa na Bakari Mwamnyeto ambayo iliruhusu jumla ya mabao 21.
Bingwa
Hapa sasa timu 16 zote zinapiga hesabu kwa sasa kusepa na taji la ligi ambalo lipo mikononi mwa Simba iliyotwaa taji hilo msimu uliopita. Ikumbukwe kwamba ilikusanya jumla ya pointi 83 baada ya kucheza mechi 34.
Namba mbili ilikuwa mikononi mwa Yanga iliyokusanya pointi 74 huku ile ya tatu ikiwa kwa Azam FC iliyokusanya pointi 68.
Watakaoshuka
Hakuna namna ni lazima timu mbili zitashuka msimu utakapomeguka hivyo jambo la msingi ni kila timu kuchanga karata zake vema ili kuweza kupata ushindi.
Mbeya Kwanza na Geita Gold ni zile ambazo zimepanda msimu huu na zinapaswa zijipange sawasawa kwa kuwa ukishuka kurudi kwenye ligi huwa inahitaji akili kubwa.
Watakaopanda pia watajulikana mwisho wa msimu hivyo na kwenye Championship ni muhimu kwa timu zote kuweza kupambana kusaka ushindi.
Toa upuuzi hapa
ReplyDelete