NYOTA Meddie Kagere amezidi kumkosha Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes kutokana na uwezo wake ndani ya uwanja jambo ambalo linamaanisha kwamba atapewa nafasi ya kutosha msimu huu kuanza kikosi cha kwanza zaidi.
Kagere ambaye ni mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara misimu miwili mfululizo 2018/19 na 2019/20, alifunga bao hilo la kwanza kwa Simba msimu huu baada ya timu hiyo kucheza mechi mbili bila ya kufunga kwenye Ngao ya Jamii na mchezo mmoja wa Ligi Kuu Bara.
Mshambuliaji huyo anayetajwa kutumia nguvu na akili kuwamaliza wapinzani, aliimalizia vema pasi ya kichwa na Chris Mugalu na kumchambua kipa wa Dodoma Jiji akiuweka mpira kimiani.
Gomes ameliambia Spoti Xtra kwamba, tayari ameusoma ushindani uliopo ndani ya Ligi Kuu Bara msimu huu, hivyo kufuatia namna ya uchezaji wa timu pinzani, ameahidi kuhakikisha anatumia washambuliaji wenye nguvu kama ilivyo kwa Kagere ili kuendana na hali ya ushindani.
“Tulianza kwa kusuasua kutokana na kutoijua ligi ya mwaka huu ndiyo maana tulipata shida kubwa mbele ya Biashara United, ila mchezo wetu na Dodoma Jiji, pamoja na kupata pointi tatu, pia tumejua mwenendo wa ligi kwa jumla, hivyo nitahakikisha natumia wachezaji wenye nguvu kwenye michezo ijayo.
“Nafahamu vizuri uchezaji wa Polisi Tanzania ambao tutakutana nao katika mchezo ujao, nitahakikisha nawaandaa zaidi nyota wangu kupambana kwa nguvu ili kulinda hali hii ya kujikuta tunatumia nguvu nyingi zaidi kupata ushindi, maana wapinzani wetu wanatumia nguvu ili kutubana,” alisema Gomes.
Bao lake mbele ya Dodoma Jiji ndani ya Ligi Kuu Bara linamfanya nyota huyo afikishe jumla ya mabao 59 ndani ya Ligi Kuu Bara.
KAGERE ANAWEZA KUWA MFUNGAJI BORA ENDAPO ATAPEWA NAFASI ZAIDI
ReplyDelete