OKTOBA 3 ilikuwa ni taarifa njema kwa wapenda michezo Tanzania baada ya kuona miongoni mwa waamuzi ambao watachezesha mechi za kimataifa pia wapo na wale ambao wanatoka Tanzania.
Hii inatoa picha kwamba taratibu waamuzi wetu wanazidi kuwa imara katika kusimamia sheria 17 katika hili ni muhimu kuwapa pongezi na wanapaswa kuendelea hapo ambapo wamefika kwenda mbali zaidi.
Zile kelele ambazo zimekuwa zikipigwa kwamba hakuna waamuzi Tanzania taratibu zitaanza kupungua ikiwa tu wale ambao wamechaguliwa wataepuka ile michezo michafu ambayo imekuwa inatajwa kuwaondoa kwenye reli.
Imani yangu ni kuona kwamba kila ambaye amepata nafasi anakwenda kuitumia na kufanya kazi kwa umakini.
Lipo wazi kwamba changamoto za makosa madogomadogo huwezi kuyakosa kwa kuwa ni lazima itokee kutokana na asili ya binadamu.
Furaha kubwa iwe kwa waamuzi kutimiza majukumu yao bila mashaka na waongeze hali ya kujiamini na kucheza zaidi na sheria na sio porojo hasa ukizingatia kwamba mpira ni mchezo ambao unapendwa hivyo furaha isiharibiwe.
Waamuzi wa Tanzania tena vijana ambao wamekuwa wakifanya vizuri kwenye mechi za ndani licha ya kunyooshewa vidole wameweza kupata nafasi.
Orodha imewataja Ramadhani Kayoko, Frank Komba, Soud Lila na Elly Sasii kwamba hawa wameteuliwa na CAF kuchezesha mchezo wa Kombe la Shirikisho barani Afrika kati ya Cffa (Madagascar) na Grupo Desportivo Interclube (Angola).
Mchezo huo utakachezwa Uwanja wa Mahamasina, Madagascar, Oktoba 17,2021 basi ni hatua nzuri na imani yetu ni kwamba mtapeperusha bendera ya Tanzania kwa umakini.
Kila la kheri na tunaona kwamba hata kwa upande wa waamuzi Wanawake nao wamekuwa wakifanya vizuri hii ni picha nzuri kwa kuwa waamuzi ni sehemu muhimu kwenye michezo.
Imeandikwa na Dizo_Click.
0 COMMENTS:
Post a Comment