*Yaelezwa
aliacha kazi ya ufagiaji na kushawishiwa
Na
Mwandishi Wetu
Maisha mazuri
kwa mshambuliaji wa zamani wa Simba, Joseph Kaniki ‘Golota’ sasa ni ndoto kwa
kuwa huenda akafungwa miaka saba au zaidi kama atakutwa na hatia baada ya
kukamatwa na madawa ya kulevya nchini Ethiopia, Alhamisi iliyopita.
Kama hiyo haitoshi,
Kaniki hataruhusiwa kuingia barani Ulaya tena kwa kuwa makazi yake yalikuwa
nchini Sweden na siku chache zilizopita, serikali ya nchi hiyo ilikuwa imempa
kibali cha kuishi nchini humo kwa miaka mitano.
Kwa mujibu
wa sheria za Sweden, aliyepewa kibali cha kuishi akikamatwa na madawa ya
kulevya, basi mara moja anapokonywa na kuzuiwa kuingia tena katika mipaka ya
nchi hiyo milele na mara moja taarifa inatolewa kwa nchi nyingine za Ulaya, iwe
hivyo.
Alivyokamatwa:
Alikuwa na
Mkwanda Matumla ambaye wakiwa Ethiopia alifanikiwa kuvuka katika sehemu za
ukaguzi hadi kwenye ndege, mbwa akamnasa Kaniki.
Baada ya
kupatikana na madawa hayo ambayo awali yalielezwa ni kilo tano, aliuruka mzigo
na kusema alimbebea Mkwanda ambaye ‘alichomolewa’ kwenye ndege na kukutwa ana
mzigo pia.
Uchunguzi
ukaanza mara moja na wakashikiliwa na kitengo cha kupambana na madawa katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole jijini Addis Ababa kabla ya kuhamishwa.
Habari za
uhakika kutoka Sweden zinaeleza, Kaniki alikuwa akiishi nyumbani kwa Mkwanda
katika mji wa Norrkoping takribani kilomita 200 kutoka mji mkuu wa Stockholm na
kazi yake kubwa ilikuwa ni ufagiaji.
“Alikuwa
akifanya kazi katika kampuni ya ufagizi (ufagiaji) hapa Norrkoping, kuna siku
tuligundua ameanza kuuza unga na alisema kwamba alipewa na rafiki yake ambaye
ni Mtanzania anayeishi Brazil.
“Kaniki
alisema rafiki yake huyo ambaye alikataa kumtaja alikuwa akiingiza unga Sweden
kupitia Tanzania. Siku chache baadaye akaacha kazi ya ufagizi na inaonekana
aliingia kwenye kusafirisha unga, maana safari zilikuwa haziishi kurudi
Afrika,” kilieleza chanzo cha uhakika kutoka Sweden.
Kwa mara ya
kwanza, miaka minne iliyopita, Kaniki alikwenda kufanya majaribio ya kucheza
soka la kulipwa katika Klabu ya Kalmar FF, akafeli na Haruna Moshi ‘Boban’
akapasi, lakini wakashindwa kuelewana, akaenda kujiunga na Gefle IF.
Mpenzi:
Kutokana na
kufeli, ingawa alikuwa hataki lakini hakuwa na ujanja, akarejea nyumbani. Baada
ya miezi kadhaa akarudi tena Sweden ambako alipata mpenzi mwenye umri zaidi ya
miaka 50.
Alirejea
Sweden baada ya mpenzi huyo kumfuata nchini, lakini si chini ya zaidi ya miezi
kumi, wakawa wameachana, kila mmoja akimshutumu mwenzake ndiye chanzo,
akachukua hamsini zake.
Soka:
Akiwa Sweden,
aliendelea kutafuta timu ya kuichezea na baada ya miezi kadhaa akafanikiwa
kusajiliwa na timu ya daraja la pili ya Konya Spor akiwa pamoja na Mtanzania
mwingine aliyewahi kuichezea Simba, William John.
Hata hivyo,
Kaniki hakuweza kupata mafanikio akiwa na Konya kutokana na kushindwa kuonyesha
kiwango, lakini yeye akalaumu timu haikuwa makini.
Kaniki alilalamika kwamba timu hiyo haikuwa
ikimlipa vizuri hivyo akaamua kuachana nayo na kutafuta maisha kivyake.
Msaada:
Maisha yake
yalikuwa ya kutangatanga huku akikaa kwa rafiki zake, wakati fulani aliishi na
Mtanzania mwingine aliyekuwa anacheza soka huko lakini baadaye ikaelezwa
alimfukuza kwake.
Mtanzania
huyo alimuamuru Kaniki kuondoka kwake kwa madai alikuwa na tabia ya kutotaka
kushirikiana na wenzake katika suala la usafi na masuala mengine.
Kazi:
Kutokana na
ugumu wa maisha, Kaniki aliamua kuhama Stockholm na kwenda Norrkoping ambako
alianza kuishi pamoja na Mkwanda Matumla.
Inaelezwa
pamoja na kufanya kazi hiyo ya ufagiaji katika majengo mbalimbali yaliyoingia
mkataba na kampuni iliyomuajiri, lakini bado maisha yalikuwa magumu kwake.
Inaelezwa
hicho ndicho chanzo cha kuamua kuingia kwenye biashara hiyo haramu na inaelezwa
alianza na kuuza rejareja katika eneo lake la kazi.
Ndani ya
Dar:
Kama
Championi Jumatatu lilivyoeleza lilipoandika kwa mara ya kwanza habari yake,
Kaniki alirejea jijini Dar hivi karibuni na kuonyesha jeuri ya fedha kila
alipokwenda.
Moja ni ile
ya kumwaga zaidi ya shilingi milioni mbili kwenye ukumbi ambao bendi ya FM
Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’ ilikuwa inatumbuiza.
Rais wa FM
Academia, Nyoshi El Saadat ‘Sauti ya Simba’, jana alithibitisha kwamba Kaniki
aliwatembelea.
“Kweli
tulikuwa naye kwenye shoo ya kule Mbezi, Kaniki ni mtu wa Ngwasuma sana na
rafiki yangu. Alikuja pale, alicheza sana siku ile na alitoa fedha nyingi
kututuza kutokana na kazi nzuri.”
Taarifa
nyingine kutoka vyanzo mbalimbali zinaeleza, baada ya kurudi nchini akitokea
Sweden wiki kadhaa zilizopita, Kaniki alimalizia ujenzi wa nyumba yake na
kununua gari jipya.
Timu:
Mwanzoni
mwa miaka ya 2000, Kaniki amewahi kung’ara akiwa na Simba. Lakini pia alifanya
vizuri akiwa mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Rayon Sports ya Rwanda na timu ya
taifa, Taifa Stars.
Wakati
fulani aliwahi kuwaniwa na Yanga na kuzua mtafaruku mkubwa, mashabiki zaidi ya
2000 wa Yanga wakajitokeza kwenye Uwanja wa Kaunda kumshuhudia akitua Jangwani
baada ya uongozi kutangaza.
Lakini
Kaniki aliyekuwa amefanya mazungumzo na uongozi huo, alibadili mwelekeo na
kurejea makao makuu ya Simba pale Msimbazi na kesho yake stori kubwa kwenye
vyombo vya habari ikawa ni namna Golota alivyowaacha wazi Yanga wakimsubiri
hadi kiza kinaingia.
Sifa yake
kubwa ilikuwa ni upigaji mashuti makali ingawa hakuwa fundi kwa upande wa
kontroo.
SOURCE:
CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment