Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) limewapeleka wanamichezo 12 wakiwemo viongozi, makocha na
wachezaji kwenye Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu
kutokana na matukio mbalimbali kwenye Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na michuano
ya Kombe la Taifa la Wanawake.
Wachezaji Dihe Makonga, Swalehe
Idd Hussein, Ramadhan Mwinyimbegu na Shaibu Nayopa wa Oljoro JKT, na Nassib
Lugusha wa Polisi Dodoma wanalalmikiwa katika Kamati ya Nidhamu kwa kushambulia
waamuzi na kufanya vurugu kwenye benchi la timu pinzani katika mechi zao za
FDL.
Mtunza Vifaa (Kit Manager) wa
Polisi Mara, Clement Kajeri analalamikiwa kwa kuongoza mashambulizi dhidi ya
waamuzi kwenye mechi kati ya timu yake na Mwadui iliyochezwa Uwanja wa
Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.
Naye Mtunza Vifaa (Kit Manager)
wa Rhino Rangers, Albert Mbunji anapelekwa katika Kamati hiyo kwa kupinga
maamuzi na kuwatukana waamuzi kwenye mechi dhidi ya Polisi Dodoma iliyochezwa
Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Pia Mtunza Vifaa (Kit Manager)
wa Oljoro JKT, Eliud Justine Mjarifu analalamikiwa kwa matukio mawili; alimpiga
Kocha wa Burkina Faso, CR Mwakambaya kwenye mechi ya FDL iliyochezwa Uwanja wa
Jamhuri mjini Morogoro. Pia alimtukana mwamuzi akiba (fouth official) Mussa
Magogo kwenye mechi dhidi ya Toto Africans iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba
jijini Mwanza.
Kocha wa Polisi Tabora, Kim
Christopher analalamikiwa kwa kumtolea mlugha chafu mwamuzi wa mechi kati ya
timu yake na Panone FC iliyochezwa Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.
Msimamizi wa Kituo cha Musoma,
Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara (FAM), Mugisha Galibona naye
anapelekwa katika Kamati ya Nidhamu kwa tuhuma za kutotoa ushirikiano kwa
maofisa wa mechi na kuchochea maofisa hao (waamuzi) kupigwa.
Kwa upande wake, Kamati ya Mpira
wa Miguu wa Wanawake ya TFF imependekeza Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu
Mkoa wa Simiyu, Emmanuel Sologo, na Kaimu Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu
Mkoa wa Singida (SIREFA), Gabriel Gunda kupelekwa kwenye kamati ya Nidhamu kwa
matukio mbalimbali yaliyojitokeza kwenye mechi za Kombe la Taifa la Wanawake.
Sologo anatuhumiwa kumpiga kibao
mwamuzi wa mechi ya marudiano kati ya timu yake ya Simiyu na Shinyanga
iliyochezwa mjini Shinyanga, tukio ambalo lilimfanya mwamuzi huyo avunje
mchezo.
Naye Gunda analalamikiwa kwa
kushindwa kuhakikisha timu yake ya Singida inaingia uwanjani kwenye mechi ya
marudiano dhidi ya Dodoma iliyokuwa ifanyike kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.
0 COMMENTS:
Post a Comment