Straika mpya wa kikosi cha Yanga, Malimi Busungu, ambaye amejiunga
hivi karibuni na klabu hiyo, ametamka wazi kuwa, licha ya kutambua ushindani wa
namba uliopo katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo, haogopi kitu kwa kuwa
anaamini uwezo wake.
Busungu ambaye anaimudu vyema nafasi ya ushambuliaji, ametua Yanga
kwa mkataba wa miaka miwili huku akifanikiwa kulamba milioni 25 kama fedha za
usajili ambapo akiwa ndani ya uzi wa klabu hiyo, anatarajia kukumbana na
upinzani mkali kutoka kwa straika mwenzake, Mrundi, Amissi Tambwe.
Busungu alisema kuwa licha ya kutambua ugumu wa kumuondoa Tambwe
ndani ya kikosi cha kwanza, lakini anaamini kuwa ataweza kufanikiwa katika
jambo hilo kutokana na uwezo wake.
“Ninafahamu jinsi ushindani wa namba katika kikosi cha kwanza
ulivyo hapa Yanga ambapo washambuliaji wake wapo katika viwango vya hali ya juu
ambapo wote tulishuhudia jinsi walivyokuwa wanapachika mabao, hasa Tambwe
ambaye alimaliza juu yangu.
“Ila mimi sina hofu yoyote ya kuingia katika kikosi cha kwanza kwa
sababu ninaamini juu ya kiwango changu ambapo nitafanya jitihada kubwa ya
kuweza kumshawishi kocha katika mazoezi ili anipange katika kikosi cha kwanza,”
alisema Busungu.
Tambwe alifanikiwa kufunga mabao 14 msimu ulioisha na kuwa
amemzidi Busungu kwa mabao matano lakini straika huyo amesema atapambana mpaka
kieleweke.
0 COMMENTS:
Post a Comment