Shirikisho
la Mpira wa Miguu nchini TFF leo limezindua jezi mpya za timu za Taifa,
zitakazokuwa zikitumika na timu za Taifa katika michuano mbali mbali itakayokua
inazikabili.
Uzinduzi
huo wa jezi mpya uliofanyika katika ukumbi wa Kilimanjaro jengo la Golden
Jubilee uliambatana na uziduzi wa tovuti mpya ya shirikisho, uliongozwa na
mgeni rasmi Mh. Said Mtanda, mbunge wa jimbo la Mchinga na Mwenyekiti wa Kamati
ya Bunge ya Maendeleo ya jamii.
Katika
uzinduzi huo, kulizunduliwa jezi aina tatu, ambazo ni jezi za ugenini, jezi za
nyumbani na jezi zitakazokuwa zikitumika kwa ajili ya mazoezi.
Ifuatayo
ni hotuba ya Rais wa TFF , Jamal Malinzi aliyoisoma wakati wa uzinduzi wa jezi
mpya za timu za Taifa, uzinduzi wa tovuti mpya ya TFF na kutunuku vyeti kwa
viongozi mbalimbali, makocha, wachezaji na wadhamini.
Mh Said Mtanda Mbunge wa Jimbo la Mchinga na Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii
Mzee Said el Maamry Mwenyekiti Msataafu wa FAT
Ndugu Leodeger Tenga Mjumbe wa Kamati ya utendaji ya CAF na Rais
mstaafu wa TFF
Ndugu wageni waalikwa
Ndugu waandishi wa habari
Mabibi na mabwana
Salam aleikum.
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa
kutufikisha hapa leo na kwa mafanikio mbali mbali ambayo tumekuwa
tukiyapata.Ninakushukuru sana ndugu mgeni rasmi kwa kuacha shughuli zako kuja
kujiunga nasi asubuhi hii katika shughuli hii.
Ndugu mgeni rasmi,tarehe 08 oktoba 1964 Tanzania ilipata
uanachama rasmi wa shirikisho la mpira wa miguu duniani FIFA. TFF tuliona jambo
zito kama hili hatuwezi kuliacha lipite hivi hivi.Hivyo mwaka jana tuliamua
kuenzi maadhimisho ya miaka 50 ya kujiunga na FIFA kwa kufanya mambo
mambo matatu makubwa.
La kwanza ni kutoa vyeti maalum kwa watu binafsi na taasisi
mbali mbali kwa kutambua mchango wao uliotukuka katika kuendeleza mpira wa
miguu Tanzania.
Leo hii ndugu mgeni rasmi tutakuomba ukabidhi vyeti hivi kwa
wawakilishi wa makundi kadhaa kwa niaba ya wenzao.Makundi haya ni pamoja na
viongozi wa kitaifa wastaafu,mawaziri wa michezo wastaafu,viongozi waliopita wa
TFF?
FAT,wakurugenzi wa idara ya michezo,wenyeviti na makatibu wa
baraza la michezo la taifa,Timuya Taifa iliyocheza fainali za Afrika mwaka
1980,waamuzi,makocha,wachezaji wa timu ya Taifa na watangazaji mahiri wa
michezo.Jumla tumetunuku vyeti 194.
Kiuhalisia idadi hii ni ndogo sana ukilinganisha na wingi na
uzito wa michango ya wadau mbali mbali wa mpira katika miaka 50
iliyopita.
Tunaomba Watanzania wenzetu watuelewe katika hili kuwa hawa
tutakaowatunuku vyeti hivi ni wawakalilisha wa wadau wote wa mpira
Tanzania.
Ninaomba tusimame kwa muda mfupi tuwaombe ewadau wenzetu na
viongozi wa mpira wa miguu ambao wako katika orodha hii na wametangulia mbele
ya haki.
Ndugu mgeni rasmi katika kuenzi miaka 50 ya Tanzania kujiunga na
FIFA leo hii pia tutatoa mchango wa fedha kwa makundi yenye mahitaji katika
jamii.
Pesa hizi zinatokana na makusanyo mbali mbali ikiwemo makusanyo
ya mechi ya ngao ya hisani ifanyikayo kila mwaka. Makundi haya ni pamoja na
walemavu wa viuongo,walemavu wa ngozi na wasioona.
Kitendo hii ni moja ya juhudi za TFF kurudisha katika jamii kile
tunachokusanya. Kila kundi litapewa shilingi milioni tano na tunaendelea
kupokea maombi toka makundi mbali ya kijamii na tukiyapitisha tutaendelea
kugawa fedha hizi.
Jambo la tatu tutakalolifanya leo litakuwa ni kuzindua rasmi
tovuti mpya ya TFF (www.tff.or.tz).
Tumeamua kufanya jamabo hili katika kuenzi miaka hamsini ya kujiunga na FIFA
ili kutoa msisitizo kuwa sasa TFF na sisi tunajiunga Na kuendeleza mpira kisasa
kulingana na teknolojia iliyopo.
Kupitia tovuti hii wadau wa mpira watapata fursa ya
kuhabarishwana kuelimishwa nkuhusu masuala mbali mbali yahusuyo mpira wa
miguu.
Tovuti hii itakuwa pia na sehemu ya kumbu kumbu (archive)
zihusuzo historia ya mpira wa miguu na matukio mbali mbali katika historia ya
mpira wetu.
Tunaomba wadau wenye kumbu kumbu mbali za mpira kama
picha,takwimu,vipande vya magazeti ya zamani na kadhalika mtuletee ili
viingizwe katika tovuti yetu.
Tunaamini tovuti hii itakuwa ndio chanzo kikuu cha taarifa na
rekodi mbali mbali za sasa na za zamani zihusuzo mpira wa miguu.
Ndugu mgeni rasmi shughuli ya leo tutaihitimisha kwa kuzindua jezi
mpya ya timu ya Taifa. Jezi hizi zitakuwa ni mbili moja ya ugenini na nyingine
ya nyumbani.Tunawapongeza watanzania wote walioshiriki katika kubuni jezi na
mwisho tuliunganisha ubunifu tofauti na kupata jezi itakayozinduliwa leo.
Ubunifu huu tayari umetafutiwa hati miliki Brela hivyo TFF
tutalinda hakii hii kwa kuwakamata na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria
wale wote watakaodiriki kuchapisha na kuuza kwa magendo jezi hizi.Utaratibu
unafanyika kumpata msambaji mmoja halali atakayesambaza jezi hizi nchini kwa
ajili ya wapenzi wa mpira wa miguu.Ukinunua jezi hii utakuwa umechangia
maendeleo ya mpira wa miguu.
TFF inawashukuru na kuwapongeza sana Tanzania Breweries
ltd ambao ndio wazalishaji wa bia ya Kilimanjaro Lager kwa sapoti wanayoitia
kwa timu ya Taifa na kutuwezesha kubuni na kuzalisha jezi hizi.Tunawashukuru
sana.
Ndugu mgeni rasmi ninaomba nimalizie kwa kuzungumzia kwa kifupi
program yetu ya mpira wa vijana.kwa kutambua umuhimu wa kuendeleza soka la
vijana TFF tumejipanga vilivyo kwa mpambano wa hatua za awali za kucheza
fainali za vijana za Afrika umri chini ya miaka 17 mwaka 2017.
Mechi za ufaulu zitafanyika kati kati ya mwaka 2016.TFF tayari
tumeunda kikosi cha awali cha vijana chini ya umri wa miaka 15 kujiandaa na
michuano hii.Kikosi hiki kimetokana na michuano ya copa coca cola ya mwaka
jana.
Tunapenda tuchukue fursa hii kumshukuru Rais Dr Jakaya Mrisho
Kikwete kwa kufanikisha nchi yetu ya Tanzania,kwa mara ya kwanza katika
historia ya nchi hii,kupata uenyeji wa fainali za Afrika. Shirikisho la mpira
wa miguu Afrika CAF limeipatia Tanzania uenyeji wa fainali za Afrika za vijana
umri chini ya miaka 17 mwaka 2019.
Tunaomba Serikali itushike mkono katika hili ili tuweze kuandaa
mashindano mazuri.Lakini haitakuwa vyema Tanzania kuandaa mashindano mazuri
lakini tukatolewa hatua ya makundi.Siku ya jumapili tarehe 07/juni TFF
tutazindua mashindano ya taifa ya vijana umri chini ya miaka 13 mjini mwanza.
Wachezaji bora wa mashindano haya ndio wataunda kikosi cha
awali cha Taifa kwa ajili ya kushiriki fainali za Afrika watoto umri chini ya
miaka 17 mwaka 2109.
Tunaomba Serikali pamoja na wadau wote tushirikiane katika
kukilea kikosi hiki ili mwaka 2019 tuwe na timu nzuri.
Tunamshukuru Mh Dr Fennela Mukangara na wizara nzima ya habari
vijana utamaduni na michezo kwa ushirikiano wanaotupatia katika hatua hizi na
katika shughuli nyingine za kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu.
Ndugu mgeni rasmi ninaomba sasa nikukaribishe uhutubie
hafla hii na pia utuongoze katika shughuli zitakazofuata.
Ahsate sana
Jamal Malinzi
Dar es salaam
03/juni/2015
0 COMMENTS:
Post a Comment