Mabingwa wapya wa Kombe la Kagame ni Azam FC, hii
wala sia hadithi mpya na tutaendelea kusema hongera kwao.
Utaona kuna ambao hawajapenda mfano wale Wakenya
ambao walikuwa wakisambaza maneno ya uzushi kwenye mitandao, kwamba Azam FC
imenunua ubingwa.
Kawaida ni watu wenye husda, wasioamini Tanzania
inaweza ikafanya jambo bora. Kikubwa kama nilivyoeleza awali ni kuwapuuza.
Mmoja wa viongozi ambao wamekuwa wakijitahidi
kusaidia michezo nchini ni Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Ameonyesha hilo kwa
dhati mbele ya wapenda soka, kikapu, netiboli na michezo mingine.
Serikali yake, haina mapenzi ya wazi na mchezo wa
soka. Unaweza kusema imejitahidi lakini hakuna mpangilio mzuri wa kusaidia soka
na michezo mingine.
Siku chache zimepita tokea Azam FC ilipofika
Ikulu kwenye kumuonyesha Kombe la Kagame Rais Kikwete. Kombe ambalo wamelibeba
kwa historia ya aina yake.
Azam FC imebeba kombe hilo kwa mara ya kwanza
bila ya kupoteza hata mchezo mmoja, timu iliyobahatika kuepuka kipigo ndani ya
dakika 90 ni Yanga pekee ambayo walikutana nayo kwenye robo fainali.
Wakati wanamkabidhi kombe hilo Kikwete aliwaeleza
mambo kadhaa, lakini moja ulikuwa ni msisitizo wake kuhusiana na suala la
kuhakikisha hawaishii Afrika Mashariki na Kati.
Kikwete aliwaeleza Azam FC mambo mengi kadhaa
ambayo ni muhimu sana kuhusiana na suala la walipofikia na likiwemo lile na
kutokubali kuwa matawi ya YAnga na Simba.
Hawajawa matawi, wamekuwa washindani ndiyo maana
leo wamefikia hapo na huenda wana nafasi nzuri ya kufika mbali zaidi ya hapo.
Maneno ya Kikwete kwamba Azam FC wasione wamefika
kwa kutwaa ubingwa wa Kagame ni jambo bora ambalo linapaswa kubaki kwenye
vichwa vya viongozi, wachezaji na hata mashabiki.
Azam FC imeanza vizuri, imefikia sehemu nzuri na
inaweza kufika zaidi ya hapo ilipo lakini kama itakuwa na watu wanaotaka kweli
kupiga hatua na kufikia mbali.
Afrika ndiyo nyumbani kwa Azam FC, mafanikio
yanaweza kupatikana kwa kiwango cha juu kama ushindani utatangulizwa na klabu
hiyo itajiamini inaweza kufika.
Kikubwa kusimamia malengo, kwamba uongozi unataka
ambacho umekianzisha. Ujiamini kwamba unaweza kufanya zaidi ya zilivyofanya
Yanga na Simba.
Hakuna ubishi itahitaji muda kwa kuwa Yanga na
Simba ni wakongwe, wametokea mbali. Lakini miaka kumi ijayo, Azam FC itaanza
kuhesabu pia imetoka mbali.
Huenda utakuwa pia ni wakati mzuri wa kuanza
kupiga hesabu ya mafanikio yake, imechukua vikombe vingapi na imefikia wapi.
Hivyo, muda hausubiri, maneno ya Kikwete yabaki
kama chachu ya kuikumbusha Azam FC kwamba haijafika na haipaswi kuwa na woga
hata kidogo. Hivyo iendelee kupambana hadi kieleweke.
0 COMMENTS:
Post a Comment