Na Saleh Ally, Kartepe
Taifa Stars imepoteza mechi yake ya kirafiki ya
mazoezi dhidi ya Libya kwa kufungwa bao 2-1.
Mechi hiyo maalum kwa ajili ya mazoezi ambayo haitambuliki na Fifa wala Caf ilifanyika katika moja ya viwanja vya hoteli ya The Green Park hapa Kartepe, Uturuki ambako Stars imeweka kambi ya kujifua.
Bao la ushindi la Libya lilikuwa ni zawadi
kutokana na kosa la kipa Said Mohammed Nduda aliyeingia kipindi cha pili
kuchukua nafasi ya Ally Mustapha ‘Barthez’.
Nduda ambaye ndiyo alikuwa ametumia dakika nne tu
uwanjani, mpira ulimpontoka mara baada ya kuudaka, wakati anajaribu kutoa pasi,
akatoa fupi iliyomfikia fowadi aliyekuwa karibu yake na kufunga kiulauni kwa
kuwa mabeki walishapanda wakiamini ameushaudaka.
Libya ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao katika
dakika ya 26 baada ya Libya kufanya shambulizi kali.
Bao hilo lilidumu hadi mapumziko huku Libya
wakilazimika kujilinda zaidi mwishoni mwa kipindi cha kwanza.
John Bocco aliisawazishia Stars bao katika dakika
ya 58 baada ya Simon Msuva kuangushwa katika eneo la boksi.
Baada ya hapo Stars ilikuwa moto kwa kushambulia
mfululizo huku Libya wakijilinda zaidi.
Huku ikionekana kama Stars ingeibuka na ushinda
kosa la Nduda liliipa nafasi Libya kupata bao la pili hivyo kuilazimisha karibu
timu nzima ya Libya kurudi nyuma na kulinda.
Mara mbili Ibrahim Ajibu aliyeingia kuchukua
nafasi ya Said Ndemla, Simon Msuva Rashid Mandawa aliyeingia kuchukua nafasi ya
Bocco wangekuwa makini wangeweza kuipatia Stars bao.
Mchezaji mmoja wa Libya alilambwa kadi nyekundu
zikiwa zimebaki dakika 12. Hiyo ilikuwa ni baada ya kumpiga kiwiko Mudathir
Yahya aliyekuwa ameingia kuchukua nafasi ya Frank Domayo.
Stars iliendelea kutawala kipindi cha pili huku
Libya inayefundishwa na kocha gwiji kutoka Hispania, Lazaro Clemente ikitumia
muda mwingi kujilinda na kubutua mipira hovyo.
STARS... |
LIBYA |
0 COMMENTS:
Post a Comment