Wakati Simba ikiwa kambini Zanzibar, watani wao Yanga nao wameamua kwenda visiwani humo kwa kambi ya mwisho kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Bara.
Hilo limezua mjadala kwa nini timu hizo kongwe zenye upinzani mkubwa zimeamua kufuatana Zanzibar na imekuwa ikionekana kama huko ni maeneo ya Simba.
Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro amezungumza na SALEHJEMBE na kuelezea sababu muhimu za Yanga kwenda Zanzibar.
"Tulichoangalia sisi ni utulivu wa kambi na uhakika wa sehemu za mazoezi. Lakini tumeangalia zaidi suala la kusogeza timu karibu na Wanayanga.
"Zanzibar ni sehemu yenye wanachama na mashabiki wengi wa Yanga, kihistoria Yanga ina mengi yanasomeka kutoka Zanzibar.
"Hata ukiangalia katika kikosi chetu tuna zaidi ya wachezaji wanne kutoka Zanzibar. Hivyo Zanzibar ni nyumbani kwa Yanga, kuweka kambi huko si tatizo hata kidogo," alisema Muro.
Yanga itafungua Ligi Kuu Bara Septemba 13 ambayo ni Jumapili kwa kuwa mwenyeji wa Coastal Union.
0 COMMENTS:
Post a Comment