Ili kuhakikisha anapunguza presha ya
mechi dhidi ya Azam FC, Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm,
ameendelea kukiimarisha kikosi chake kwa kuwapa mbinu mbalimbali zitakazowapa
ushindi wa mapema kwenye mchezo huo.
Timu hiyo, imeweka kambi yake huko Landmark
Hotel jijini Dar es Salaam huku ikiendelea kujifua kwenye Uwanja wa Boko
Veterani.
Yanga na Azam FC zinatarajiwa kujitupa
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar kuvaana katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayopigwa
Jumamosi hii.
Kocha huyo, katika
mazoezi ya juzi Jumatatu, alionekana akiwataka wachezaji wake kucheza soka la
kasi huku wakishambulia muda mwingi.
Pluijm amesema kikubwa anawapa mafunzo
wachezaji wake ya kucheza soka la pasi za haraka wakati wanashambulia lango la
timu pinzani ili apate ushindi wa mapema.
“Kama unavyojua hivi sasa nipo
kwenye maandalizi ya mechi dhidi ya Azam, hivyo ninaendelea kuziboresha baadhi
ya nafasi, ikiwemo ya ushambuliaji ili kuhakikisha ninapata ushindi wa mapema
kwa ajili ya kupunguza presha ya mechi.
“Yanga hivi sasa inapaniwa sana, hiyo ni
kutokana na kila timu kutaka kutufunga, hivyo hali hiyo inasababisha presha ya
mechi kuwa kubwa ndani ya uwanja.
“Ili presha ya mechi ipungue, basi
nipate ushindi wa mapema ili wachezaji wangu wacheze kwa kujiamini na hilo
linawezekana kutokana na maandalizi ninayoyafanya,” alisema Pluijm.
0 COMMENTS:
Post a Comment