Kocha Mkuu wa Simba, Dylan Kerr, licha ya kuwepo kwa taarifa kuwa anaweza kutimuliwa ndani ya kikosi hicho na nafasi yake kupewa kocha wa zamani wa timu hiyo, Mserbia, Goran Kopunovoc, ameibuka na kusema suala hilo wala halimtishi hata kidogo.
Hivi karibuni kuliibuka taarifa za ndani ya Simba zikisema uongozi umempa Muingereza huyo michezo ya mzunguko wa kwanza iliyobakia kuhakikisha anapata matokeo mazuri la sivyo anaweza kuondolewa kukioongoza kikosi hicho.
Kerr alisema anachojiamini ni kwamba kazi yake anaifanya ipasavyo hivyo hata akitimuliwa ni kama wanamuonea tu.
"Hilo suala la kuondolewa wala halinitishi hata kidogo, nimekuwa nikiifanya kazi yangu kwa ufanisi lakini mazingira yanatunyima kufanikiwa na kupata ushindi.
"Kabla ya mechi yetu na Mwadui tulikua tukifanya mazoezi kwenye uwanja mbovu ambao ni kama sehemu ya malisho ya ng'ombe, kocha unatakiwa kuiandaa timu katika hali nzuri ili mpate matokeo mazuri. Pia siku moja kabla ya mechi tulikwenda uwanjani tukaukuta haupo katika kiwango kizuri.
"Binafsi hata mimi matokeo haya yananiumiza, mashabiki wengi kutoka Dar walikuja kutusapoti lakini wameondoka vichwa chini, baada ya mchezo nilimuona mwanadada akilia kwa uchungu kisa hatujapata ushindi, hiyo inaonyesha ni jinsi gani mashabiki wanaumizwa na matokeo mabaya," alisema Kerr.
Sare iliyoipata Simba, juzi Jumamosi ni ya tatu mfululizo, ilianza kutoka sare ya 2-2 dhidi ya Azam kisha ikaambulia 1-1 na Toto Africans.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment