January 27, 2016


BONIFACE WAMBURA, BOSI WA BODI YA LIGI...

Na Saleh Ally
TUKITAKA kubadilika, kuendelea na kutoka hapa tulipo, kwanza kabisa lazima tukubali kufungua mioyo yetu tukiwa kizani na kusema hili ni baya au hili ni sahihi.

Lakini tujenge utamaduni wa kukubali, lakini tumalize kila kitu kwa kumuogopa Mungu hata kama tunaamini hajali au haupendi mpira.

Mpira wa Tanzania unavurugwa na Watanzania wenyewe, mpira wa Tanzania hauwezi kuwa na mafanikio kwa kuwa Watanzania wenyewe hawayataki mafanikio.

 Haitatokea hata siku moja kila Mtanzania akaenda kuongoza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au kila mmoja akapata nafasi ya kuwa kiongozi wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB).

 Kuna watu wachache watapewa dhamana ili kushikilia uongozi wa gurudumu la maendeleo la mchezo husika. Hawa watu lazima wakubali kwamba wao ni watumishi wa umma.


RAIS WA TFF, JAMAL MALINZI
 Nasisitiza tena, wafanyakazi wote wa TFF na TPLB ni watumishi wa umma. TFF ni yangu mimi, wewe na Watanzania wote. Si ya mtu binafsi, hivyo utendaji wao lazima uiangalie jamii ya Watanzania na si kuitumikia Fifa- Shirikisho la Soka la Kimataifa ambalo limejaa kashfa rundo. Tunaona, hakuna kiongozi wake hata mmoja wa juu anayeonekana kusalimika kama utazungumzia usafi.

TFF na TPLB, kweli wanaweza kuamua wanavyotaka kwa kuwa tu ni viongozi? Mara ngapi nimekosoa na kuonekana mbaya lakini sijajali, huenda sasa ifikie mahali waone haya!

Angalia mgogoro huu mpya katika soka nchini, mgogoro ambao unaweza kuuita ni wa kipuuzi kabisa lakini unagundua kwamba TFF ni watu ambao si makini, halikadhalika TPLB ambao ni sehemu kuu ya usimamizi wa ligi kuu.


 Unaweza kukataa kama kweli ligi hiyo sasa haina mvuto kwa maana ya masuala ya kitaalamu na ufundi. Moja, haina watu sahihi wanaoongoza mashindano. Nilishasema kuhusiana na uwezo wa mkurugenzi wa mashindano, kwamba hana sifa, hili sikuwa ninatania.

Lakini bado inaonekana TPLB hawako makini, hawako tayari kuona kuna ligi yenye mpangilio wa maana na unaoeleweka. Ligi ya sasa ina viraka rundo kwa kuwa kila baada ya muda mfupi inaahirishwa.

 Kila baada ya mechi mbili, tatu nne, inasimama na inategemea inaweza kuwa sababu za msingi au za kijinga kama ambazo sasa zinaonekana zitasababisha ligi hiyo kusimama.

Unategemea vipi kuwa na wachezaji bora kwa ajili ya kuunga kikosi bora cha timu ya taifa, Taifa Stars wakiwa wanatokea katika ligi ya kuungauunga kama hii ya sasa?

 Azam FC wameomba kwenda kushiriki mashindano nchini Zambia, eti TFF ikakubali na kuwapa nafasi waondoke na mechi zao za ligi zitasogezwa mbele!
Nchi gani inaweza kufanya upuuzi kama huo, kisingizio eti Azam FC itaiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho. Wale waliopanga ratiba hawakulijua hilo? Azam FC hawakuyajua mashindano hayo kabla? Kama wameyajua juzi, vipi TFF au TPLB wakubali kuahirisha ligi kienyeji namna hiyo?

 Kuna utaratibu maalum na siku ambazo timu zinaweza kuingia katika maandalizi, zinajulikana. Leo TFF au TPLB wameamua tu! Yanga nao wanaonekana kutokubali, wameanzisha safari ya Afrika Kusini, wamesema wanakwenda kuweka kambi ya zaidi ya siku tano.

 Utagundua Yanga wala hawakuwa na mpango wa kwenda, kisa ni Azam FC. Simba nao wameona ni vizuri kwenda Kenya, eti wana michuano fulani hivi wamealikwa. Baada ya hapo kila timu inataka kwenda inapotaka.
 Hilo pekee linaonyesha kiasi gani timu zimechoka, tena zimechoka kwa kuwa zimeona zinaongozwa na viongozi wasiojua umuhimu wa ligi, wasiojua au kuona huruma ya gharama kwa klabu.

Inawezekana kuwa na klabu bila ya TFF, lakini ni vigumu kuwa na TFF bila klabu au timu. Sasa shirikisho hilo linapaswa kujali na kuheshimu mateso ya klabu hizo zinazopambana kuwalipa wachezaji, kuwagharimia, kuwaandaa kwa kuwa zinatoa fedha nyingi.

 Hata hivyo, vunja kambi, anza upya kila mara ni gharama. Lakini kiufundi ni kupoteza momentum (kasi ya mwendelezo kimchezo). Kwani ni kawaida ya mwili kisayansi, ukisimama utaendelea taratibu na timu zitakazoathirika zaidi ni zile ndogondogo hasa ligi inaposimama bila sababu za msingi. Timu kubwa, nazo huathirika kwa gharama.

 TFF na TPLB wao ni kama bluetooth tu, zinanyonya fedha kwenye kila mkataba kwa kuzitumia klabu. Hivyo zijenge heshima na kuonyesha thamani kwenye klabu. Ziongoze kwa usawa na kuanza kuondoa hisia tofauti zinazojenga hisia za kwamba upande fulani unapendelewa.

Lakini nilisema tangu awali, TFF wanapaswa kuwa na wataalamu sahihi ambao watajua kusimama kwa ligi kunaathiri nini, watu sahihi ambao wataongoza mashindano wakiwa na uwezo na uzoefu na si wale waliowekwa ilimradi tu.

 Kuiruhusu Azam FC haikuwa sahihi, ligi ya nchi haiwezi kusimamishwa au kusimamisha mechi za timu eti ikashiriki michuano tena isiyotambuliwa na Fifa wala Caf yaani Shirikisho la Soka Afrika.


Ligi hiyo imekuwa ikisimama kwa ajili ya Kombe la Kagame ambalo lina heshima yake. Sasa basi imetosha na lazima TFF na TPLB, sasa wabadilike, waone haya, waone huruma na wafanye mambo kitaalamu. Waungwana mmelipua sana, basi imetosha, eeh!

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic