May 13, 2016

SABO (KATIKATI) AKISHANGILIA MOJA YA MABAO ALIYOFUNGA.

Kiungo wa Coastal Union ya Tanga, Yussouf Sabo, raia wa Cameroon, ametamka wazi kuwa anatamani siku moja aweze kuichezea timu kubwa hapa nchini kati ya Simba au Yanga, lakini kuna jambo moja ambalo linamfanya apate ugumu huo.

Sabo ambaye ni kiungo wa juu anayetumia mguu wa kushoto, aliwahi kufanya majaribio na kikosi cha Yanga kabla ya kujiunga na Coastal mwanzoni mwa msimu huu.

Kumekuwa na taarifa kwamba Simba imekuwa ikimfuatilia kiungo huyo kimyakimya na hiyo ni baada ya kuitungua kwenye mchezo wa robo fainali ya Kombe la FA na kuitupa nje kwa mabao 2-0 ambayo yote aliyafunga yeye. Upande wake amesema hana tatizo kama wakimfuata.

“Unajua sisi wachezaji wa kigeni tunaocheza timu hizi ndogo tunapata wakati mgumu sana wa kusajiliwa na timu kubwa kwa sababu ya wao kuhofia uwezo wetu kama utaendelea kuwa juu au la, lakini pia kwenye masuala ya kutuhudumia kama unavyojua sisi wageni tuna mambo mengi tofauti na wachezaji wa hapa Tanzania.

“Hivyo timu hizo zinaogopa kuingia gharama halafu mwisho wa siku mchezaji anakuwa hana msaada, lakini hilo halinikatishi tamaa.

“Nimepanga Juni 2, mwaka huu niende nyumbani Cameroon kurekebisha mambo yangu kisha nikirudi naamini hapo nitajua nianzie wapi harakati za kutafuta timu ya kuichezea msimu ujao japo lengo langu ni kubaki Tanzania kuichezea timu kubwa mojawapo kati ya Simba au Yanga,” alisema Sabo.

Sabo aliongeza kuwa, kwa sasa wanaishi maisha yasiyoridhisha ndani ya klabu yao ya Coastal kwani hakuna fedha za kuendesha maisha yao huku timu hiyo ikiwa tayari imeshuka daraja kutoka Ligi Kuu Bara mpaka Ligi Daraja la Kwanza.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV