May 14, 2016Zikiwa zimebaki siku 14 tu kabla ya tamasha la kila mwaka la Majimaji Selebuka 2016 kuanza Mei 28, mwaka huu mjini Songea, waratibu wa tamasha hilo bado wanasaka udhamini kwa ajili ya kufanikisha lengo lao.

Tamasha hilo linaloratibiwa na Asasi ya Songea & Mississippi (Somi) litachukua muda wa wiki nzima katika Uwanja wa Makumbusho ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji uliopo Songea Mjini ambapo zinahitajika Sh milioni 45 ili lifanyike kikamilifu.

Mratibu wa tamasha hilo,  Reinafrida Rwezaura ameliambia Championi Jumamosi kuwa, lengo la tamasha hilo ni kuinua vipaji, kutangaza utalii wa Mkoa wa Ruvuma pamoja na kumuinua mwananchi wa chini kupitia maonyesho na mafunzo ya ujasiriamali yatakayokuwepo.

Pia kutakuwa na mashindano ya riadha, mbio za baiskeli ambapo kutakuwa na washiriki kutoka mataifa mbalimbali, ‘debate’ kwa shule za sekondari, utalii wa ndani na ngoma za asili.

“Kwa niaba ya asasi nipongeze kampuni zilizojitokeza kutusapoti mpaka sasa, lakini bado tunahitaji udhamini zaidi ili kutimiza azma yetu. Tunaomba kampuni na watu binafsi kutusapoti,” alisema Rwezaura.


Mpaka sasa tamasha hilo limefanikiwa kupigwa jeki na Kampuni ya Bakhresa, Global Publishers, CRDB, Chuo Kikuu Huria (Open University) na blogu namba moja ya michezo nchini ya Saleh Jembe.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV