May 14, 2016

WENGER


Na Saleh Ally
LEO hii ni miaka 19 na siku 230 tangu Kocha Arsene Wenger ajiunge na kikosi cha Arsenal akitokea Nagoya Grampus ya Japan.

Hii leo, pia ni miaka 12 na siku 21, tangu Arsenal ichukue mara ya mwisho ubingwa wa Ligi Kuu England.

Wenger ameiwezesha Arsenal kubeba ubingwa England mara tatu katika misimu ya 1997-98, 2001-02 na 2003-04 ambao ulikuwa wa mwisho.

Wenger amefanikiwa kubeba ubingwa wa Kombe la FA mara sita ambayo mara ya mwisho ilikuwa ni msimu wa 2014-15, si mbali.

Ukizungumzia ngao za jamii, Wenger ameiongoza Arsenal kuchukua mara sita pia. Mara ya mwisho ilikuwa ni 2015, yaani mwaka jana tu.

Kama utasema sherehe za kushangilia kushinda kombe au ngao kwa Arsenal chini ya Wenger zimefanyika mara 15. Hii ni katika kipindi cha miaka 20 ambayo amekaa na klabu hiyo.

MSUVA

Lakini mashabiki wengi wa Arsenal wakiwemo wale wa hapa nyumbani Tanzania, wanachotaka ni kuona Wenger anaondoka kwenye klabu hiyo.

Hakika hawataki kumuona na hawana sababu kubwa ambayo inawasukuma kufanya hivyo, isipokuwa ni ubingwa wa England pekee.


Kombe la FA, ni msimu mmoja tu uliopita. Ngao ya Jamii ni mwaka mmoja uliopita, lakini ubingwa Ligi Kuu England, sasa ni miaka 12, hiki ndicho chanzo cha majonzi, lawama, masikitiko na hasira za mashabiki wa Arsenal.

Mashabiki wa Arsenal ambao walikuwa na miaka mitano wakati Arsenal inachukua ubingwa mara ya mwisho sasa ni watu wazima.

Mashabiki waliokuwa na umri wa miaka sita, wakisindikizwa na wazazi wao kwenda kuanza darasa la kwanza kwa mara ya kwanza, sasa wako katika chuo kikuu kama walijiendeleza kielimu, au ni wafanyabishara wanaojitegemea kama waliamua kuanza biashara mapema.

Kwa wasichana mashabiki wa Arsenal waliokuwa na umri wa miaka 10 hadi 15 Arsenal ilipobeba ubingwa Ligi Kuu England, asilimia kubwa sasa watakuwa na familia zao wakiitwa mama au Mrs Nanihiii.

Msuva ana umri wa miaka 22 sasa, wakati Arsenal inatwaa ubingwa England mara ya mwisho alikuwa ana umri wa miaka 10, akiwa nyumbani chini ya baba Msuva. Sasa ana kwake, ana gari lake pia ni staa wa Yanga na Taifa Stars! Hii ndiyo vita kubwa ya wanaoipenda Arsenal, wanajiona kama wanasimangwa sana.


Juhudi za Wenger zinaonekana kuwa zimeishia kuipeleka timu kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya pekee. Yaani kugombea nafasi nne za juu tu. Tena ikionekana kama watabeba ubingwa kila mwishoni mwa ligi, wanaharibu, wanachukua nafasi ‘walizozizoea’.

Wakati Arsenal wanataka Wenger aondoke, kuna kila sababu ya kujiuliza, kweli Wenger aondoke na ikiwa hivyo wamejiandaa kweli na yupi hasa wanamwamini!

Kikubwa cha kuangalia, wapinzani wao wengine, Manchester United, sasa wanahaha. Kila kocha ni mbaya baada ya kuondoka kwa Sir. Alex Ferguson ambaye ndiye pekee anamzidi Wenger mafanikio kwa makocha waliopo.

Arsenal ni timu inayotaka kocha wa kuendelea kubaki angalau kwa miaka 10. Si kama Jose Mourinho anataka afanye yake na kuondoka fasta. Nani atawasaidia Arsenal, wana uhakika?

Viongozi na wamiliki wa Arsenal wamekuwa waoga, wanajua madhara ya hilo kwa kuwa tayari Wenger ana utamaduni wa Arsenal. Kila akikosea katika ubingwa, anawapa nafasi ya kushiriki ligi ya mabingwa, wanaingiza fedha.


Bado ameanza kuingia kwenye makombe kama hivyo msimu uliopita kutwaa ubingwa wa Kombe la FA. Kamwe hawawezi kumuondoa na shabiki anayetaka Wenger aondoke baada ya msimu huu, ‘atajimaliza kwa presha’. Vizuri asubiri msimu ujao ambao atalazimika pia kuangalia, kweli aende au la!

Kwa Wenger mwenyewe, pia analazimika kubadilika.

Usajili:
Amekuwa mgumu kutoa fedha, msimu uliopita alibadilika lakini mara nyingi anapenda bei chee.

Mfano aliwasajili Petr Cech, Alexis Sanchez na Mesut Ozil, pekee alioonekana amepatia lakini usajili wa wengine kama sita au saba, ukawa hauna faida na hasara kwa Arsenal. Hili amekuwa akilirudia sana.


Kudekeza:
Amekuwa akikinga mgongo wake hata wachezaji wanapoharibu, hii inawafanya wadeke na kujisahau.

Ukweli ni hivi, lazima awe mkali na wanapokosea basi waelezwe ukweli na wajue, Arsenal ina mashabiki wanaoumia.

Kupuuza:
Wachezaji wake wengi wanaonekana kujali zaidi mechi kubwa kama zile za Man United, Chelsea lakini zile dhidi ya Swansea, Norwich City, wanazipuuza na ndiyo zinawaangusha mwisho.

Mfumo:
Amekubali kubadilika kidogo, lakini bado anatakiwa kuufanyia kazi mfumo wake anaouamini sana wa 4-2-3-1.


Msimu wa 2003-04, alitwaa ubingwa wa England bila ya kufungwa katika mechi 49, wakabandikwa jina la ‘Invisibles’, lakini sasa wanaonekana kuwa laini mwishoni kwa kuwa mambo yamebadilika, basi aache ubishi. Eeeh!

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV