July 11, 2016

JULIO

Na Saleh Ally
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limetangaza kutakuwa na hafla ya kukabidhi tuzo mbalimbali za washindi wa Ligi Kuu ya Bara kwa msimu wa 2015-16.

Hafla hiyo imepangwa kufanyika Julai 17, mwaka huu jijini Dar es Salaam na tuzo 13 zitatolewa.

Kamati ya Tuzo ya TFF ndiyo itaratibu zoezi la mwisho kuwatangaza washindi ambao tayari wachache wameingia kwenye fainali.

Hii haitakuwa mara ya kwanza kufanyika kwa tuzo hizo ambazo mwisho ni zile zinazotoa mwelekeo wa ligi ya msimu uliopita ilivyokuwa na ujao, watu wapambane vipi.
Makosa yamekuwa yakionekana kama ada kwa kuwa uteuzi wa wale wanaowania tuzo inakuwa kama ndani yake kuna siasa.

Nasema siasa kwa kuwa kuna hali ya kuridhishana, Usimba na Uyanga, kuangalia nani asichukie au kina fulani wakiwemo, watu watachukizwa.

 Tuzo zitakuwa ni hizi, mabingwa, makamu bingwa, mshindi wa tatu, mshindi wa nne, timu yenye nidhamu, mfungaji bora, mchezaji bora wa ligi, kipa bora, kocha bora, mchezaji bora chipukizi, mchezaji bora wa kigeni, bao bora la msimu na mwamuzi bora.

Hapa kuna aina mbili za tuzo, kwanza ni zile ambazo tayari zimepatikana kama mfungaji bora, bingwa, nafasi ya pili na kadhalika. Pili ni zile ambazo watawania watu wawili au watatu kupata mmoja na hizo ndiyo tatizo kubwa.

Unapokwenda kwenye mchezaji bora utaona kuna wachezaji watatu ambao ni Shiza Kichuya (Mtibwa Sugar), Juma Abdul (Yanga) na Mohamed Hussein Zimbwe (Simba). Jiulize, kweli Shomari Kapombe au Aishi Manula wa Azam FC, hakuna aliyestahili kuingia hapa?


Nitakupa mfano, Shomari Kapombe kaisaidia Azam FC kushika nafasi ya pili ikiwa na pointi 64 na yeye akafunga mabao nane sawa na Kichuya ambaye ameisaidia Mtibwa Sugar kukamata nafasi ya tano ikiwa na pointi 50!

Pamoja na kuisaidia Azam FC kushika nafasi ya pili na kufunga mabao 8 akiwazidi washambuliaji kibao. Kapombe kafunga mabao mengi kuliko Zimbwe ambaye ana moja. Sasa kigezo hapa ni nini hasa? Au ni lazima kwa kuwa wapo Simba, lazima uchague mmoja wa Yanga?

Acha nikukumbushe, Kapombe ni mchezaji bora wa Januari, Abdul Aprili. Zimbwe au Tshabalala hakushinda yoyote na hiyo ni fainali pia ni lazima itaamuliwa pia na ushindani wa ushindi wa mwezi. Sasa kaingiaje, au ndiyo kuipoza Simba?

Kwenye kipa bora, unaona Angban anawania tuzo ya mchezaji bora wa kigeni anaingia kama kipa. Lakini kwenye tuzo ya kipa bora hayumo, hili ni tatizo jingine la kiufundi.

Siamini kama tuzo za mwezi ambazo zinatolewa na yuleyule anayetoa za msimu haziwezi kuwa na maana katika ushindi wa mwisho. Kama ni hivyo, hili ni jipu.

Pia nina mjadala wa kumchukua Mecky Maxime na kumuacha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’. Huyu anaachwa kwa kuwa anasema ‘hovyo’, anasema kweli au akishinda au kuingia ‘atapata sifa’.

Julio aliipandisha timu yake misimu miwili, ule wa kwanza ikapokwa pointi mezani, msimu uliopita ikapanda tena na moja kwa moja imemaliza msimu ikiwa katika nafasi ya sita.


Mtibwa Sugar ambayo ni ‘kizee’ wa Ligi Kuu Bara, imeshika nafasi ya tano na Mwadui ambayo imepanda msimu mmoja na moja kwa moja imeenda hadi nafasi ya sita.

Tena Julio ameonyesha kwamba wachezaji wanaodharauliwa kwa kuvikwa uzee, wanaweza kufanya vizuri. Kama utaniambia ni kigezo cha pointi, basi angeingia Hans va Der Pluijm na Stewart Hall ambaye bado anahesabika alifanya kazi msimu huo.

Msimu mmoja umepita, Mbwana Makata alipewa kocha bora baada ya kuisaidia Prisons kutokana na kutopoteza hata mechi moja katika nane za mwisho. Sasa timu imepanda daraja na kushika nafasi ya sita, huyu si kocha bora? 
Waliopanda na Mwadui ni Majimaji, iko nafasi ya kumi, Toto walishika nafasi ya 13 na African Sports, wakateremka daraja.

Hapa ni sehemu ya kuonyesha namna gani mambo hayaendi kiufundi na badala yake kuna sehemu inaendeshwa na matakwa ya wahusika au kutokubali kwa kazi ya fulani kwa kuwa anajisifia sana au atamkera fulani.

Angalia kipengele cha mchezaji bora chipukizi, wako Farid Mussa (Azam), Mohamed Zimbwe (Simba), Mzamiru Yasin (Mtibwa Sugar) na Shiza Kichuya (Mtibwa Sugar). Vipi kuhusu Raphael Alpha ambaye ameisaidia timu yake, pia takwimu zinaonyesha ni kiungo bora kabisa mkabaji kwa vijana kipindi hiki kama ilivyo kwa Mudathiri Yahaya wa Azam FC.

Ni sababu hakuna anayemfuatilia Alpha au hadi Yanga au Simba. TFF inahofia kuweka wachezaji wa Azam FC sababu ya kuonekana kuna ufananishaji wa jambo kwa kuwa Azam TV ni wadhamini wa ligi hiyo? Na kama ni hivyo wanaona kweli wanatenda haki?


Kipengele cha wachezaji bora wa kigeni wako Donald Ngoma na Thabani Kamusoko (wote Yanga) na kipa Vincent Angban (Simba), raia wa Ivory Coast. Kweli mfungaji bora haingii hapa, au kwa kuwa tayari ana tuzo mkononi ndiyo maana ameachwa ili ‘kubalansi’?

Amissi Tambwe amefunga mabao 21 na kuweka rekodi ya kurejesha washambuliaji kufunga mabao zaidi ya 20 kwa msimu mmoja, hii ilipita zaidi ya misimu minne wote wakifunga chini ya mabao 20.

Lakini ukiangalia tuzo za mchezaji bora wa mwezi, kuanzia Septemba 2015 hadi Mei, 2016, mchezaji wa kigeni aliyeshinda tuzo ya mwezi ni Kamusoko pekee. Hao wengine wameingiaje, ipi ni sahihi? Kama hawajakosewa, kipi kimewaingiza?

Lakini bado ninahoji, unapozungumzia mchezaji bora wa ligi, kwani wale wa kimataifa hawapaswi kuingia. Ligi inashirikisha wote.

TFF hawakuona kunapaswa kuwa na vipengele vitatu vya ubora ambavyo ni mchezaji bora mzalendo, bora wa kigeni halafu wachanganywe kupata mchezaji bora wa ligi.

Kama watashinda wageni, huenda itakuwa ni changamoto kwa wazalendo kuchangamka. Kuliko kurahisisha mambo, jambo ambalo si sawa kabisa.

Lengo ni kujenga, imefikia hatua TFF walifanye hili suala kitaalamu zaidi na kuachana na kuangalia sababu ambazo zinakuwa nje ya uwanja.
Tuzo hizo ni za ndani ya uwanja na si suala la kiungozi. Hivyo hakuna suala la ‘kubalansi’, kama mchezaji anastahili tuzo tano na apewe tu kwa kuwa ni haki yake. Ikiendelea hivi, hata hii maana ya tuzo itakuwa haina maana utakuwa ni mgawo wa kuridhishana na si kufuata sahihi kinachotakiwa.
Mchezaji Bora:
Shiza Kichuya (Mtibwa Sugar)
Juma Abdul (Yanga)
Mohamed Hussein (Simba) 

Kipa Bora:
Aishi Manula (Azam)
Beno Kakolanya (Tanzania Prisons)
Deogratius Munishi (Yanga)

Kocha Bora:
Hans van Der Pluijm (Yanga)
Mecky Maxime (Mtibwa Sugar)
Salum Mayanga (Tanzania Prisons)

Mchezaji bora Chipukizi:
Farid Mussa (Azam)
Mohamed Hussein (Simba)
Mzamiru Yasin (Mtibwa Sugar)
Shiza Kichuya (Mtibwa Sugar)

Mchezaji bora wa Kigeni:
Donald Ngoma (Yanga) 
Thabani Kamusoko (Yanga)
Vincent Angban (Simba)

Waamuzi Bora:
Anthony Kayombo
Ngole Mwangole
Rajab Mrope.

WACHEZAJI BORA WA MWEZI:
Hamisi Kiiza-SEPTEMBA, Simba
Elias Maguri-OKTOBA, Stand
Thabani Kamusoko-DESEMBA, Yanga 
Shomari Kapombe-JANUARI, Azam
Mohamed Mkopi-FEBRUARI, Prisons
Shiza Kichuya-MACHI, Mtibwa
Juma Abdul-APRILI, Yanga
Abdulrahman Mussa- MEI, JKT Ruvu

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV